Katibu wa Halmashauri kuu ya chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa itikadi na uenezi Shaka Hamdu Shaka amewataka wakala wa chakula Mkoa wa Ruvuma (NFRA) kuweka utaratibu mzuri ili kumaliza utata uliopo juu ya zoezi la ununuzi wa mahindi Manispaa ya Songea.
Hayo yalibainishwa wakati alipotembelea kituo cha wakala wa chakula Taifa (NFRA) kilichopo ndani ya Manispaa ya Songea hapo jana tarehe 20 Septemba 2021 wakati akihitimisha ziara yake ya siku mbili Mkoani Ruvuma kwa lengo la kukagua miradi ya Maendeleo ambayo ni utekelezaji wa ILANI ya CCM.
Shaka alisema kuwa wakala wa chakula (NFRA) ahakikishe wananchi wote ambao wameorodheshwa idadi ya mahindi yao, yananunuliwa kwa wakati pamoja na kuongezwa kwa kituo kingine cha ununuzi wa mahindi ili kupunguza msongamano katika kituo kinachotumika sasa na kuondoa usumbufu kwa wananchi.’Alisisitiza’
Aliongeza kuwa Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 50 kwa ajili ya ununuzi wa mahindi na amewaahidi wakulima Tani thelathini na tano elfu za mahindi zitanunuliwa mwaka huu katika Mkoa wa Ruvuma pamoja na kutafuta masoko nje ya Nchi.
Pia alitembelea mradi wa ujenzi wa bwalo la sekondari ya Emmanuel Nchimbi ambapo aliahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 30 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mradi huo sambasamba na Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt. Damas Ndumbaro naye aliahidi kutoa shilingi milioni 20 kwa lengo la kukamilisha kiasi kilichobakia kumaliza ujenzi wa bwalo hilo ambacho kilikuwa ni shilingi milioni 50.
Shaka alihitimisha ziara yake katika Mkoa wa Ruvuma kwa kutembelea mradi wa ujenzi wa madarasa 2, ofisi 1 na ukamilishaji wa madarasa 3 katika shule ya msingi Amani iliyopo kata ya Mjimwema Manispaa ya Songea pamoja na mradi wa ujenzi wa boksi kalavati na barabara ya BP station-Sangawani ya KM 1.1 kwa kiwango cha lami nyepesi na kuridhishwa na ukamilishwaji wa miradi hiyo.
IMETOLEWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
21.09.2021
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa