UTUMIKISHAJI watoto wadogo bado unaendelea nchini, licha ya serikali kuweka sheria ya kumlinda mtoto mwenye umri usiozidi miaka 18.Nimepita katika baadhi ya maeneo mjini Songea na kubaini watoto wenye umri kati ya miaka tisa na 12 ambao wanazunguka kuuza bidhaa ndogo ndogo na wengine wanaombaomba.
Said Ally ni mtoto anayesoma darasa la pili katika shule moja katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambaye anafanya biashara ya kuuza karanga za kukaanga.“Nimeanza biashara hii tangu darasa la kwanza nikitoka shuleni saa tano nafika mjini kuuza karanga katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya klabu za pombe,hadi kufika saa tisa nakuwa nimemaliza kuuza karanga ambapo kwa siku Napata sh. 5000’’,anasema.
Anadai pesa anayopata inamsaidia yeye na mama na wadogo zake kuendesha maisha kila siku,ingawa amekiri kuwa inamwathiri katika masomo yake kwa kuwa hapati muda wa kutosha kushiriki katika masomo.Uchunguzi ambao nimeufanya katika viunga vya mji wa Songea majira ya usiku kuanzia saa mbili hadi saa tano usiku nimeshuhudia watoto wadogo wakifanyabiashara hatarishi kutokana na mazingira.
Tatizo la kuwatumikisha watoto wadogo kazi halifanyiki kwa ajili ya biashara pekee bali pia watoto wameonekana wakifanyishwa kazi katika maeneo mengine kama vile maeneo ya machimbo,kazi za ndani na uvuvi,kuponda kokoto na kufanyishwa vibarua.
Sheria ya haki za mtoto ya mwaka 2009, inabainisha wazi kuwa mtu hataruhusiwa kumuajiri au kumshughulisha mtoto katika aina yoyote ya kazi itakayomnyonya mtoto.Kwa mujibu wa sheria hiyo,mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya kutengwa au matendo yoyote yanayoweza kuwa na athari mbaya kwake kwa kuzingatia umri na uwezo wake.Tanzania ni miongoni mwa nchi 174 zilizoridhia Azimio la Umoja wa Mataifa namba 182 la kukomesha utumikishaji watoto chini ya umri wa miaka 18.
Makala haya yameandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Julai 16,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa