Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
21 MACHI 2022
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro (MB) amempongeza Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mapinduzi ya maendeleo ndani ya sekta ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania.
Amebainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Ruvuma hapo jana Machi 20, 2022 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea kwa lengo la kueleza mambo 10 muhimu yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha siku 365 tangu aingie madarakani.
Alisema kuwa Serikali ya awamu ya sita imeongeza juhudi katika kuimarisha uhifadhi rasilimali za wanyama pori ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja ujangili umepungua kwa asilimia 90% na kupelekea ongezeko kubwa la idadi ya Faru katika hifadhi mbalimbali nchini.
“Sekta ya Maliasili na Utalii imechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la mapato na uchumi wa Taifa ambapo kwa kipindi cha siku 365 idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka kwenye watalii 562,549 hadi kufikia watalii 788,933 sawa na ongezeko la asilimia 40.2% na kuongeza mapato kutoka kwenye Bilioni 9.7 hadi Bilioni 12.4 kwa watalii wa ndani tu” Dkt. Ndumbaro alibainisha.
Aliongeza kuwa licha ya dunia kukumbwa na janga la UVIKO 19 hali iliyopelekea kushuka kwa shughuli za utalii kwa mataifa mengi, kwa nchi ya Tanzania idadi ya watalii kutoka nje imeongezeka kwa asilimia 48.6% na hivyo kuongeza mapato kutoka kwenye dola za kimarekani Milioni 714. 59 hadi kufikia dola za kimarekani Bilioni 1 sawa na asilimia 76%.
Serikali ya Awamu ya sita imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 90.2 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu katika maeneo ya hifadhi za Utalii pamoja na kutoa mafunzo mbalimbali kwa wadau pamoja na waongoza utalii nchini ambapo watu 150 kutoka kila Mkoa walipata fursa ya kushiriki mafunzo hayo.’Alieleza’
Dkt. Ndumbaro alisema kuwa “Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo kwa kila Mkoa kuhakikisha wanaandaa matamasha ya utamaduni kwa lengo la kutoa chachu na kutangaza utalii ambapo kwa Mkoa wa Ruvuma Tamasha la Majimaji Serebuka litaanza kufanyika kimkoa pamoja na kuanzisha kumbukizi ya miaka 100 ya Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ili kuchochea uzalendo na kuibua miradi mbalimbali hasa katika maeneo ya hifadhi za Utalii”.
Pia, Serikali imefanikiwa kutafuta masoko ya Utalii nje na ndani ya nchi kwa kipindi cha siku 365 na kufanikiwa kuuza zaidi ya vitalu 79 vya uwindaji kwa mfumo wa kielektroniki pamoja na kuwekeza juhudi kubwa ya kuendeleza sekta ya misitu na Nyuki kwa kuunda sheria ndogo inayoruhusu usafirishaji wa mkaa mbadala nje ya nchi pamoja na kuanzisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya Nyuki ambapo miongoni mwa wanufaika wa viwanda hivyo ni Manispaa ya Songea.
Alieleza kuwa Nchi ya Tanzania imefanikiwa kutambulika na kupewa heshima katika nyanja ya Utalii duniani kwa kupokea Tuzo zaidi ya kumi kutoka katika mashirika makubwa duniani ikiwemo na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Utalii (UNWTO) ambapo hata hivyo bado Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuendelea kuitangaza Tanzania nje na ndani ya nchi kwa kuingia mikataba na mashirika mbalimbali ya kimataifa ikiwemo na shirika la ndege la Emirates. “Alibainisha”
Ametoa rai kwa waandishi wa habari kuendelea kuhamasisha jamii katika kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Kwa upande wao waandishi wa habari wametoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Mh. Waziri kwa kusimamia vizuri utekelezaji katika sekta ya Maliasili na Utalii na kuiomba Serikali kuboresha vivutio vya Utalii vilivyopo Mkoani Ruvuma.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa