Siku ya UKIMWI Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 01 Disemba ambapo kwa Manispaa ya Songea maadhimisho hayo yamefanyika katika kata ya Ruvuma Mtaa wa Ruvuma juu katika uwanja wa Black Belt ambayo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka Roa, KONGA, Viongozi pamoja na wananchi kwa lengo la kuongeza ufahamu wa ugonjwa wa UKIMWI unaosababishwa na Virusi vya UKIMWI.
Maadhimisho hayo yanalenga kutoa fursa ya kutathimini hali halisi na mwelekeo wa kudhibiti Virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI Kitaifa na kimataifa, kutafakari changamoto, mafanikio na kuimarisha mikakati mbalimbali ya kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Akizungumza Naibu Meya Manispaa ya Songea Jeremia Mlembe kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Songea ambapo amewataka wananchi wote kuondoa unyanyapaa kwa waathirika na wagonjwa wenye maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Mhe. Jeremia amewapongeza KONGA kwa kujitolea katika kutoa elimu ya kupinga unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Virus Vya UKIMWI huku akisisitiza Halmashauri kuendelea kuiwezesha KONGA ili waweze kufikia malengo yao ya kuifikia jamii.
Aliongeza kuwa ushiriki wa jamii kwa pamoja utasaidia kuondoa dhana ya Serikali na wadau au Asasi zinazoshughulika na mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI na hatimaye kutokomeza maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI hadi ifikapo 2030.
Kwa upande wake Mratibu wa Maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani Hamprey Mbawala alisema “ kwa mwaka wa fedha julai 2022 hadi juni 2023 jumla ya watu 51,757 wamepima afya zao ikiwa wanaume ni 21,880 na wanawake 29,877 kati ya hao wanaume 512 na wanawake 943 wamekutwa na maambukizi ya VVU sawa 2.8% na wamefanikiwa kuunganishwa na huduma ya tiba na matunzo katika vituo vya kutolea huduma za VVU (CTC).
Hali ya maambukizi inaonesha kushuka kwa 1.2% ikilinganishwa na mwaka wa fedha Julai 2022 hadi juni 2023 ambapo ilikuwa ni 4.0% katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
KAULI MBIU 2023; JAMII IONGOZE KUTOKOMEZA UKIMWI”
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa