SONGEA KUTOKOMEZA MBU
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imeanza utekelezaji wa kutokomeza mbu baada ya kutoa mafunzo maalum kwa wafanyakazi wa kujitolea 49 watakaofanya kazi ya kupulizia dawa hiyo katika mazalio ya mbu yaliowazi na yaliofunikwa.Mratibu wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa wa Afya na Mazingira katika Manispaa ya Songea Vitalis Mkomela amesema kwa kuanzia zoezi hilo linafanyika katika mitaa 49 iliyopo kwenye Kata kumi za Manispaa hiyo baada ya mafunzo ya nadharia na vitendo kukamilika.
Mkomela anazitaja Kata zinazoanza kupuliziwa dawa za kutokomeza mbu kuwa ni Subira, Matarawe, Majengo, Lilambo, Mletele, Bombambili, Ruhuwiko, Mjini, Mwengemshindo na Mfaranyaki.Tayari mafunzo hayo pia yametolewa na maafisa watendaji wa mitaa na kata ambao watashirikiana na maafisa wa Afya wa Kata ambao watakuwa wasimamizi wadhibiti wa mbu katika mitaa na kata husika.
Serikali imeongeza chachu katika mapambano dhidi ya malaria baada ya kununua lita laki moja za dawa za kuua mbu na kusambazwa kote nchini ili kukabiliana na malaria.
Viuadudu vya kutokomeza mbu wa malaria vinatengenezwa katika kiwanda cha kuzalisha Viuadudu kilichopo Mjini Kibaha mkoani Pwani.Halmashauri 14 nchini ikiwemo ya Manispaa ya Songea zina viwango vikubwa vya maambukizi ya ugonjwa wa malaria,tayari Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Songea zimeanza utekelezaji wa mradi huo wa kutokomeza mbu.
Afisa Afya na mazingira wa Manispaa ya Songea Dk.Vitalis Mkomela amesema manispaa ya Songea imepokea lita 1000 za dawa hiyo ambazo zimenunuliwa na Rais Dk.John Magufuli ambapo kiasi hicho cha dawa kinatosha kupulizia kipindi hiki cha kiangazi katika mitaa 95 ya Manispaa hiyo.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa