MJI wa Songea uliopo katika Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa maeneo machache hapa nchini ambayo yana hazina kubwa ya utajiri wa kihistoria na kishujaa.
Mashujaa kutoka katika Mji wa Songea waliendeleza mapambano dhidi ya ukoloni wa Kijerumani hivyo kuchangia kikamilifu harakati za ukombozi kabla ya kupata uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.
Jina la Mji wa Songea ni kumbukumbu ya Nduna Songea ambaye alikuwa na Ikulu yake katika Mji wa Songea.Mji wa Songea una majengo ya kumbukumbu za kihistoria mbalimbali yakiwemo makanisa yenye miaka zaidi ya 100.
Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Barthazar Nyamusya anasema historia inaonesha kuwa Mji wa Songea ulianzishwa mwaka 1897 kama kituo cha kijeshi cha Kijerumani.
“Mji wa Songea uliendelea kukua na kuwa Makao makuu ya utawala wa Wajerumani katika Wilaya ya Songea,Mji huo ulizinduliwa rasmi kuwa mji wa kihistoria,kishujaa na kiutalii mwaka 2010’’,anasema Nyamusya.
Hata hivyo Nyamusya anabainisha kuwa Mji wa Songea uliathirika na Vita ya Majimaji kati ya mwaka 1905 hadi 1907 na Vita kuu ya pili ya Dunia kati ya mwaka 1939 hadi 1945.
Licha ya Mji huo kuathirika na vita hivyo,uliendelea kuwa Makao makuu ya Mkoa wa Ruvuma wakati wa utawala wa Waingereza katika Tanganyika,baada ya uhuru hadi leo bado Songea ndiyo Makao Makuu ya Mkoa wa Ruvuma.
Nyamusya anasema Mji wa Songea una umaarufu wa mashujaa wa Vita vya Majimaji ambapo mashujaa 67 walinyongwa mwaka 1906 kati yao mashujaa 66 walizikwa katika kaburi moja.
Nyamusya anabainisha kuwa Nduna Songea Mbano ambaye alikuwa na umaarufu,alinyongwa na kuzikwa katika kaburi lake ambapo makaburi yote yapo katika Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea.
Mashujaa hao 67 walinyongwa katika eneo lililojengwa Mnara wa Mashujaa wa vita vya Majimaji nyuma ya ukumbi wa Songea ambalo ni kivutio cha aina yake cha utalii katika Mji wa Songea .
Makumbusho hayo yalikabidhiwa katika Shirika la Makumbusho ya Taifa chini ya sheria ya makumbusho ya Taifa la Tanzania,namba saba ya mwaka 1980 hivyo makumbusho hayo yalipandishwa hadhi na kuwa Makumbusho ya Taifa mwaka 2010.
Tanzania ina nyumba sita za Makumbusho ya Taifa katika maeneo mbalimbali nchini ambazo Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es salaam,Kijiji cha Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam,Makumbusho ya Elimu Viumbe Arusha,Makumbusho ya Azimio la Arusha, Makumbusho ya Mwalimu Julius Nyerere Butiama na Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 13,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa