UJENZI wa zahanati ya St. Benjamini iliyopo katika Kata ya Msamala Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,ulianza Novemba 2012 na kukamilika mwaka 2014. Ujenzi wa Zahanati hii umegharimu shilingi 468,000,000.00 ambazo zimetumika kujenga na kukamilisha vyumba 16 na vyoo matundu manane.
Zahanati hiyo ilisajiliwa na kuanza kutoa huduma rasmi Machi 2017. Zahanati hii inahudumia wakazi kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya Manispaa, ambapo Jumla ya wagonjwa 345 wanapata huduma katika zahanati hiyo kwa mwezi kati yao watoto ni 75 na wakubwa ni 270.
Hata hivyo lengo la kujenga zahanati hii ni; Kusogeza huduma kwa jamii,Kupunguza msongamano wa wagonjwa hospitali ya rufaa ya Mkoa (Homso),Kutoa huduma za mama na mtoto (RCH) na wale wenye bima za Afya endapo tutakubaliwa,Kutoa huduma za uchunguzi wa tiba kwa watoto yatima wanaotunzwa katika kituo cha St. Theresa na Kutoa huduma za vipimo mbalimbali za mama wajawazito.
Akizungumza mara baada ya kuzindua zahanati hiyo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 Charles Kabeho ameagiza Mfuko wa Bima ya Afya(NIHF) kushughulikia haraka maombi ya kibali cha zahanati hiyo kutoa huduma kwa kutumia Bima ya Afya ili kuwawezesha wananchi wanaokatwa fedha zao Bima kutumia zahanati hiyo kupata huduma hivyo kupunguza msongamano katika hospitali za wilaya na Rufaa mkoani Ruvuma.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 9,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa