TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Ruvuma imebaini baadhi ya miradi katika Wilaya ya Songea kijengwa chini ya kiwango.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa TAKUKURU mkoani Ruvuma Yusta Chagaka wakati anatoa taarifa ya utendaji kazi wa TAKUKURU kwa wanahabari katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi 2019.
Kwa mujibu wa Chagaka,katika kipindi hicho TAKUKURU Ruvuma imefanya ufuatiliaji wa miradi mitano ya maendeleo ili kujiridhisha iwapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo zinatumika kadiri ilivyokusudiwa.
Ameitaja miradi iliyofuatiliwa kuwa ni mradi wa maji wa Lituta-Mtepa katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea wenye thamani ya zaidi ya milioni 546 na mradi wa mabweni mawili ya wanafunzi katika sekondari ya Mahanje Halmashauri ya Madaba wenye thamani ya shilingi milioni 150.
Miradi mingine ni upanuzi wa kituo cha Afya Muhukuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea wenye thamani ya shilingi milioni 500 na kwamba miradi yote hiyo ina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.141
Hata hivyo amesema kutokana na ufuatiliaji wa miradi hiyo,imebainika baadhi ya miradi kujengwa chini ya kiwango, baadhi ya mafundi kulipwa malipo yao yote wakati bado hawajamaliza kazi na baadhi ya miradi kuchelewa kukamilishwa kwa muda mrefu kutokana na Wizara husika kutotuma fedha za kukamilisha miradi hiyo.
Chagaka amesema katika kipindi hicho,TAKUKURU mkoani Ruvuma imeokoa mishahara hewa ya shilingi milioni 21 katika sekta ya Afya na kwamba fedha zilizookolewa zimerejeshwa serikalini.
Kwa mujibu wa Chagaka katika kipindi hicho TAKUKURU mkoani Ruvuma imepokea taarifa 75 kutoka kwa wananchi kupitia vyanzo mbalimbali na amezitaja Idara zinazoongoza kulalamikiwa kuwa ni Ardhi yenye malalamiko (12), Afya(14), Halmashauri(10), Mahakama(10),Polisi(6),Elimu(5),Vyama vya Ushirika(5), Maji(2), Ujenzi(2),TANESCO(2) na Nishati(2).
Kulingana na Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma,Idara nyingine ambazo zimelalamikiwa na wananchi ni Taasisi za Fedha,Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA),Shirika la Hifadhi ya Jamii(NSSF),TARURA,Serikali za vijiji,Pembejeo na Sekta binafsi.
“Idadi ya kesi zilizoendelea mahakamani ni kumi,katika kipindi hicho kesi mpya tano zilifunguliwa kati ya hizo mbili zilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea na moja katika Mahakama ya Wilaya ya Mbinga’’,alisema Chagaka.
Katika hatua nyingine ya utafiti na udhibiti,Mkuu huyo wa TAKUKURU Ruvuma amesema Taasisi yake,imefanyakazi ya uchambuzi wa mifumo tisa ili kubaini mianya ya rushwa katika sekta ya ulipaji kozi za majengo katika Wilaya za Songea, Mbinga,Tunduru,Namtumbo na Nyasa ambapo imebainika elimu kwa wananchi haijatolewa vya kutosha na walipa kodi wengi wameshindwa kutofautisha kati ya kodi ya majengo na kodi ya ardhi.
Amesema katika mfumo wa utoaji wa mikopo kwa vikundi vya vijana,wanawake na wenye ulemavu,katika Wilaya za Songea na Namtumbo,imebainika kuwa baadhi ya Halmashauri hazitengi asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa ajli ya mikopo hiyo.
“Imebainika baadhi ya maafisa wanaohusika,wanaomba rushwa kutoka kwa wanufaika wa mikopo hiyo au kamisheni’’,alisisitiza Chagaka.
Amesema TAKUKURU inaendelea kutoa shukrani kwa wadau wote wanaotoa ushirikiano na Taasisi yake na ametoa rai kwa wananchi wote kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa TAKUKURU.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini
Aprili 12,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa