TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Ruvuma imemfikisha mahakamani Mchumi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Sydeny Mpangala kwa makosa kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri wake na kujipatia zaidi ya shilingi milioni 1.8.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Owen Jasson, Februari,7 mwaka huu TAKUKURU ilimfikisha mtuhumiwa huyo katika mahakama ya Wilaya ya Mbinga akikabiliwa na makosa mawili.
Jasson ameyataja makosa hayo kuwa ni kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007 na kuisababishia hasara serikali kinyume na aya ya 10(1) ya jedwali la kwanza na kifungu cha 57(1) na 60(2) vya sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kulingana na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU,Machi 25,2017,TAKUKURU ilipokea taarifa kuwa Sydney Mpangala alitumia nyaraka kumdanganya mwajiri na kujipatia kiasi cha sh.1,803,510 na kwamba nyaraka hizo zilizonesha kuwa fedha hizo zilitumika kununulia vifaa mbalimbali visivyokuwa vya viwandani kwa ajili ya ujenzi wa kibanda cha Mlinzi kwenye nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo iliyopo eneo la Kipika mjini Mbinga.
“Baada ya kupokea taarifa hiyo uchunguzi ulifanyika na kukusanya ushahidi uliothibitisha kuwa mtuhumiwa alitenda makosa ya udanganyifu na kuisababishia hasara serikali,hivyo tarehe 07/02/2019,mtuhumiwa alifikishwa kwenye mahakama ya Wilaya ya Mbinga na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi namba moja ya mwaka 2019’’,alisema Jasson.
Kesi hiyo ilisomwa na Wakili wa Serikali Gregory Chisauche mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbinga Aziza Hassan Mbadjo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Februari,8,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa