TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Ruvuma imemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Tunduru Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Umoja Edwin Mlanda kwa tuhuma za kuomba rushwa ya shilingi 100,000.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Owen Jasson,Mtuhumiwa huyo anakabiliwa na makosa ya rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11,2007.
“Mnamo tarehe 22/10/2019.Ofisi ya TAKUKURU wilayani Tunduru ilipokea taarifa yenye malalamiko dhidi ya ndugu Edwin Mlanda kwamba siku ya tarehe 12/10/2019, kwa njia za rushwa aliomba na kupokea fedha sh.100,000 kutoka kwa Jemsi Amnaay’’,alisema.
Amesema Jemsi alihamia katika kijiji cha Umoja kutokea Mkoa wa Manyara ambapo Afisa Mtendaji huyo alidai kwamba Jemsi alifika kwenye kijiji hicho bila kuwa na barua kutoka Manyara inayothibitisha kwamba yeye ni raia mwema hivyo aliambiwa atoe fedha hizo ili ampatie kibali cha kuishi kwenye kijiji hicho.
Jasson amesema uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU umethibitisha kuwa mtuhumiwa alitenda makosa ya rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa hivyo alifikishwa mahakamani Novemba 8,2019.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini Manispaa ya Songea
Novemba 11,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa