TAASISI ya Kuzuia Na Kapambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Ruvuma imemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Mbinga Afisa Mtendaji wa Kata ya Linda Cosmas Nyoni akituhumiwa kwa makosa ya kuomba na kupokea fedha kwa njia ya rushwa.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Owen Jasson,Mtuhumiwa amefanya kosa kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Jasson amesema mnamo Agosti 3,2018,ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mbinga ilipokea taarifa kuwa Cosmas Nyoni kwa njia za rushwa Juni 29,2018 aliomba fedha kiasi cha shilingi 550,000 kutoka kwa Zacharia Komba ili asiweze kumchukulia hatua na kumpelekea watu wa upekuzi nyumbani kwake ili kumpekua kwa makosa ya kujihusisha na ununuzi holela wa kahawa iliyopigwa marufuku ya magoma.
“Siku hiyo Mtuhumiwa alipokea fedha kiasi cha shilingi 100,000 ikiwa ni sehemu ya fedha alizoomba na siku ya Julai 4,2018 alipokea tena fedha nyingine kiasi cha shilingi 250,000,pia ikiwa ni sehemu ya fedha alizokuwa ameomba’’,alisema Jasson.
Amesema baada ya kupokea taarifa hiyo,uchunguzi ulifanyika ambapo ilithibitika kwamba ni kweli Mtuhumiwa ametenda makosa ya rushwa ambapo Mei 17 mwaka huu,Mtuhumiwa amefikishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Mbinga na kufunguliwa kesi ya Jinai Namba 41 ya mwaka 2019.
Kulingana na Naibu Mkuu wa TAKUKURU,Kesi hiyo imesomwa na Wakili wa Serikali Chali Kadeghe mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbinga Aziza Hassan Mbadjo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini
Mei 17,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa