TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma imeokoa kiasi cha Zaidi ya shilingi milioni 53 ambazo zingetumika kama mishahara hewa katika sekta ya afya,elimu na TAMISEMI.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma kwa wanahabari katika kipindi cha kuanzia Julai 2017 hadi Juni 2018,Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Yustina Chagaka amesema kati ya fedha zilizookolewa katika sekta ya afya pekee zimeokolewa Zaidi ya shilingi milioni 44.
Kulingana na Chagaka katika sekta ya elimu zimeokolewa shilingi milioni tatu na TAMISEMI Zaidi ya shilingi milioni tano na kwamba fedha hizo zimerejeshwa serikalini na kuongeza kuwa shilingi milioni sita zimerejeshwa kwenye kikundi husika ambako zilichukuliwa kinyume cha utaratibu.
“Katika kipindi hicho majalada ya uchunguzi 45 yalifunguliwa na majalada ya uchunguzi 22 yalikamilika kuchunguzwa na kutumwa katika Mamlaka za Juu kwa mapitio,majalada yaliopelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP) kuombewa vibali vya mashtaka ni tisa na ambayo tayari yamepatiwa kibali cha mashtaka ni manne’’,anasisitiza Chagaka.
Kulingana na Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma,katika kipindi hicho TAKUKURU imepokea taarifa 298 kutoka kwa wananchi kupitia vyanzo mbalimbali ambapo amezitaja Idara zinazoongoza kulalamikiwa kuwa ni serikali za Mitaa(Ofisi ya wilaya,kata,vijiji na mitaa taarifa 70.
Idara nyingine ni Ardhi taarifa 53,Polisi 30,Mahakama 26,Kilimo 23,Elimu 19,Ujenzi 13,Afya 11,Vyama vya siasa 11,Hifadhi ya Jamii 4,Fedha 4 na Maliasili,NIDA na sekta binafsi kila mmoja imepokea malalamiko matatu.
“TAKUKURU inaendelea kuwaasa wananchi wote kushirikiana nasi katika mapambano haya kwa kukataa kujihusisha na vitendo vya vya Rushwa,kukemea vitendo vya rushwa na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa katika ofisi za TAKUKURU’’,anasisitiza Chagaka.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Agosti 2,2018
Mawasiliano albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa