Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma,katika kipindi cha kuanzia Julai 2016 hadi Machi 2017 imeokoa kiasi cha zaidi ya sh. 91 ambayo yalikuwa ni malipo hewa.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Yusta Chagaka amewaambia wanahabari ofisini kwake mjini Songea kuwa kati ya fedha hizo katika sekta ya elimu ziliokolewa zaidi ya sh.milioni 61 na sekta ya kilimo zaidi ya sh.milioni 2.2 kama mishahara hewa.
Chagaka anabainisha zaidi kuwa katika sekta ya ujenzi kiasi cha sh.milioni 28.5 ziliokolewa, na kwamba kiasi hicho cha fedha kililipwa kwa mkandarasi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Mpitimbi B hadi Mbinga Mhalule katika Halmashauri ya Songea kwa kazi ambazo hazikufanyika.
Amesema TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma katika kipindi hicho imepokea taarifa za malalamiko 173 kutoka kwa wananchi kupitia vyanzo mbalimbali.
Anazitaja idara zinazoongoza kulalamikiwa kuwa ni malalamiko 40 toka TAMISEMI,Elimu malalamiko 26, Kilimo 21, Afya 18, Ujenzi 17, Ardhi 16, Mahakama 14, Maji 10, Polisi 9 na Watu binafsi mawili.
Katika kuendelea kutekeleza jukumu la kushirikisha na kuelimisha jamii dhidi ya Rushwa Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma anasema ofisi yake Imefanya Semina 53, Mikutano ya hadhara 45 na kuanzisha Klabu 51 za wapinga rushwa katika shule za msingi, sekondari na vyuo zimeelimishwa na kuimarishwa.
Chagaka anasema katika kipindi hicho miradi ya maendeleo 12 inayohusu ujenzi wa miundombinu ya Afya, Elimu, Maji, Kilimo na mifugo yenye thamani ya zaidi ya sh.bilioni 3.5 ilikaguliwa.
Anasema baadhi ya miradi hiyo ilikuwa na viashiria vya ubadhirifu hivyo uchunguzi wa matumizi ya fedha ya miradi hiyo unaendelea na upo katika hatua mbalimbali za uchunguzi.
Anaitaja mikakati ya TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma katika kumaliza kero kwa wananchi ni kufuatilia fedha za miradi ya maendeleo kama zinatumika ipasavyo,kuendelea kufanya tafiti ndogo katika idara mabalimbali za Umma zinazolalamikiwa ili kubaini mianya ya rushwa na kupendekeza njia madhubuti za kuziba mianya hiyo kwa manufaa ya wananchi.
Mikakati mingine ni Kufanya warsha zinazohusisha wadau mbalimbali na idara zinazolalamikiwa ili kuweka mikakati ya pamoja ya kuziba na kuiondoa kabisa mianya ya rushwa katika idara husika.
Anasema TAKUKURU itaendelea kufanya uchunguzi kwa weledi ili kuhakikisha malalamiko yote yanachunguzwa ipasavyo na watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yao.
Anasisitiza TAKUKURU inajenga mahusiano madhubuti na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wanashiriki kikamilifu na kwa dhati katika mapambano dhidi ya rushwa na kuendelea kuelimisha wananchi katika ngazi mbalimbali juu ya madhara ya rushwa ili waichukie rushwa.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa