TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Ruvuma imefanya uchambuzi wa mifumo mitatu ili kubaini mianya ya rushwa katika sekta ya Elimu katika usimamizi wa mitihani ya kitaifa.
Mkuu wa TAKUKURU mkoani Ruvuma Yustina Chagaka akitoa taarifa ya utendajikazi wa TAKUKURU katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Aprili hadi Juni 2019 kwa wanahabari mjini Songea ,amesema mianya hiyo imechunguzwa katika Halmashauri za Manispaa ya Songea,Halmashauri ya Wilaya ya Songea na Madaba.
Amesema katika kipindi hoicho TAKUKURU ilifanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maazimio ya warsha ya wadau kuhusu mfumo wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na ujazaji fomu za afya kwa wanafunzi wanaoanza masomo ya sekondari katika Halmashauri za Mji Mbinga na kuokoa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 22.
Kamanda wa TAKUKURU mkoani Ruvuma Christina Chakaga ametoa wito kwa Halmashauri kutoa elimu ya sheria kwa mabaraza ya ardhi ya Kata.
Kuhusu mabaraza ya ardhi Chagaka amesema mabaraza ya ardhi ya Kata yanafanya kazi za kisheria,wakati hawana elimu ya sheria jambo linalosababisha kuongezeka kwa vitendo vya rushwa katika Idara ya ardhi wakati wa kutatua migogoro baina ya mlalamikaji na mlalamikiwa.
“Katika kipindi cha miezi mitatu TAKUKURU mkoani Ruvuma imepokea taarifa za malalamiko ya rushwa 63 toka vyanzo mbalimbali ambapo kati ya malalamiko hayo idara ya ardhi inaongoza kwa kulalamikiwa kwa malalamiko 17’’,alisema.
Ameitaja Idara inayofuatia kwa kulalamikiwa kuwa ni idara ya elimu yenye malalmiko 10 na ya mwisho kulalamikiwa ni taasisi za kifedha zenye malalamiko mawili.
Aidha TAKUKURU Ruvuma imefanya ufutiliaji wa zaidi ya shilingi bilioni 14 ambazo zimetolewa na serikali kwa ujenzi wa miradi ya miundo mbinu ya ujenzi, maji,afya,elimu na barabara nakubaini dosari ndogondogo ambazo zimeshatolewa ushauri wa wanamna ya kurekebisha dosari hizo.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika nchini baadaye mwaka huu, Chakaga amewataka wagombea na wapiga kura kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vitawasababishia matatizo ya kuchukuliwa hatua za kisheria kulingana na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 ya kuongoza vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini.
TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma imeendelea kutekeleza matakwa ya Sheria inayoongoza majukumu matatu ambayo ni kuzuia rushwa,kuelimisha umma na kuchunguza tuhuma za rushwa na kushitaki watuhumiwa.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Julai 20,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa