Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
27.01.2022
Halmashauri ya Manispaa ya Songea imefanya kikao cha baraza la Madiwani (TARURA) leo tarehe 27 Januari 2022 kwa lengo la kujadili na kupitisha mpango wa bajeti ya matengenezo ya barabara kwa mwaka 2022/2023.
Akiwasilisha bajeti hiyo Meneja wa Wakala wa barabara za vijijini na Mjini (TARURA) Wilaya ya Songea Eng. John Ambrose alisema kuwa mpango na bajeti ya matengenezo ya barabara mwaka wa fedha 2022/2023 ambao umeandaliwa kwa kuzingatia uimarishaji wa barabara ambazo tayari zilishafunguliwa, upelekaji wa huduma kwenye maeneo ya kijamii kama vile shule na zahanati pamoja na maeneo ya biashara na uzalishaji kwa kuzingatia idadi ya watumiaji wa barabara hizo.
Eng. Ambrose alibainisha kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea imepanga kutumia jumla ya shilingi 3,349,780,000.00 ili kufanyia matengenezo ya mtandao wa barabara kwa mchanganuo wa matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi, madaraja, matengenezo ya muda maalum, usimamizi wa miradi utawala, fedha za tozo, fedha za jimbo pamoja na fedha za maendeleo.
Aliongeza kuwa miongoni mwa changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2021/2022 ni pamoja na ufinyu wa bajeti ya matengenezo ya barabara, mahitaji makubwa ya ufunguzi wa barabara mpya na uharibifu wa miuondombinu ya barabara unaochangiwa na mvua, ambazo tayari wamejipanga kuzitatua katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/2023.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea ametoa pongezi kwa wataalamu na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa matengenezo ya barabara nyingi ambazo zilifanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 na amewataka TARURA Wilaya ya Songea kuhakikisha wanatatua changamoto za miundombinu katika maeneo ambayo bado hayajafanyiwa matengenezo.
Wakitoa hoja zao kuhusiana na mpango na bajeti ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Waheshimiwa Madiwani walibainisha changamoto za miundombinu ya barabara zilizopo katika maeneo yao ambapo TARURA Wilaya ya Songea imeahidi kuzifanyia matengenezo barabara hizo katika bajeti iliyowasilishwa.
Nae Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Hamisi Abdallah Ally amewataka TARURA Wilaya ya Songea kutoa ushauri wa kitaalamu kabla ya kuanza matengenezo ya barabara kulingana na bajeti iliyopangwa ili kuhakikisha wanatengeneza barabara zenye ubora na kiwango kinachotakiwa.
Bajeti hiyo ya mpango wa matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambayo imewasilishwa kwa baraza maalumu la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea imepitishwa na Madiwani hao kwa asilimia 100%.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa