WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) leo Machi 28,2018 wamekabidhi mabweni matatu na madarasa mawili ya shule ya msingi Luhira iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo na Manispaa ya Songea,Meneja wa TBA Mkoa wa Ruvuma Edwin Nunduma amesema mradi huo ulihusisha ujenzi wa mabweni matatu na ukarabati wa madarasa mawili kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 151.
Kwa mujibu wa Meneja huyo wa TBA kila bweni Lina uwezo wa kulaza wanafunzi 12 hivyo mabweni matatu yatalaza wanafunzi wenye ulemavu 36.
Mkuu wa shule hiyo Joyce Konga amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi wenye ulemavu 48 ambapo amesema baadhi ya wanafunzi wenye umri mdogo itawalazimu kulala wawili wawili.
Hata hivyo ameishukuru serikali kwa kuwajengea wanafunzi hao mabweni ya kisasa na kukarabati madarasa mawili ambayo pia yana Mazingira rafiki kwa wenye ulemavu.
Shule ya msingi Luhira ndiyo Shule pekee yenye kitengo cha wasioona mkoani Ruvuma ambayo ilianzishwa mwaka 1929 na kitengo cha wasioona kilianzishwa mwaka 1982.
Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1300 kati yao wenye ulemavu ni 48.Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme alikabidhi msaada wa magodoro 24 yenye thamani ya shilingi milioni 1.8 kwa ajili ya wanafunzi wasioona wanaosoma katika shule hiyo hivyo kumaliza tatizo la upungufu wa magodoro katika shule hiyo.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Machi 28,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa