UGONJWA wa Saratani ya Tezidume hausababishwi na maambukizi ya magonjwa ya ngono kama wengi wanavyodhani, imeelezwa.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Steven Meena amesema hayo leo alipozungumza na MTANZANIA Digital katika mahojiano maalum yaliyofanyika viwanja vya maonesho ya Sabasaba.
“Katika banda letu jumla ya wanaume 252 wamejitokeza kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya tezidume kati yao 11 walikutwa na dalili za awali za saratani hiyo,” amesema Meena.
Amesema kuwa awali maonesho hayo yalipoanza idadi ya waliojitokeza ilionekana kuwa ndogo lakini iliendelea kuongezeka kadiri siku zilivyosonga mbele.
“Wapo waliotueleza kwamba walihofia kipimo cha kidole lakini baadae idadi iliongezeka nadhani waliokuja mwanzoni walienda kuwaeleza wenzao kwamba tulikuwa tunatumia kipimo cha PSA (cha damu na si kidole,” amesema.
Ameongeza kuwa, ” Mwamko ulikuwa mkubwa na tumebaini bado jamii haina uwelewa wa kutosha kuhusu magonjwa haya ya saratani, kwa mfano walikuwa wanatuuliza iwapo saratani ya tezidume inahusiana na magonjwa ya ngono, yaani mtu anaweza kuipata kwa kushiriki ngono, jambo ambalo si sahihi, tumewaelimisha.
“Pia tulifanya uchunguzi wa saratani ya matiti kwa wanawake, tumeona jumla ya wanawake 426 kati yao watano tuliwakuta na vivimbe na mmoja tayari alikuwa na dalili za awali za saratani hii,” amesma.
Dk. Meena amesema watu wote waliokutwa na dalili za awali za saratani ya tezidume na matiti wamepewa rufaa kwenda ORCI kwa uchunguzi zaidi na tiba.
CHANZO:GAZETI LA MTANZANIA
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa