TFDA YAKAMATA MAFUTA YA ALBINO NA VYAKULA
IDARA ya Afya katika Manispaa ya Songea kwa kushirikiana na watalaam wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) wamefanya operesheni katika maduka ya vipodozi katika mji wa Songea na kufanikiwa kukamata mafuta ya albino yakiuzwa kinyume cha sheria.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea Dk.Mameritha Basike amesema mafuta hayo yalikamatwa katika duka la Godluck Mranga ambayo alikuwa anauza shilingi 4500.
“Hairuhusiwi mafuta ya kupaka Albino aina ya sunblock cream UV40 kuwepo kwenye maduka ya vipodozi badala yake mafuta hayo yanaruhusiwa kuwepo kwenye maduka ya dawa (Pharmacy)’’,anasisitiza Dk.Basike.Amesema katika duka hilo pia vimekamatwa vyakula mbalimbali vilivyoharibika vikiwemo maziwa ya kopo 12 yenye thamani ya zaidi ya sh.200,000 na nyama ya kopo 20 zenye thamani ya sh.100,000.
Afisa Afya wa Manispaa ya Songea Vitalis Mkomela amesema mfanyabiashara huyo amepigwa faini ya sh.500,000 kulingana na sheria za TFDA na kwamba ametoa rai kwa wafanyabiashara kuacha kuwauzia wananchi bidhaa ambazo zimeharibika au kumalizika muda wake.“Natoa wito kwa wananchi kabla ya kununua bidhaa yoyote wajiridhishe kwa kusoma tarehe ya kutengenezwa bidhaa na mwisho wa matumizi ili kuepuka kununua bidhaa ambazo zimeharibika zinazoweza kuleta athari kiafya kwa mtumiaji’’,anasisitiza Mkomela.
Mfamasia Wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Ndavitu Sanga anatahadharisha watu wenye ulemavu wa ngozi(Albino) katika Manispaa hiyo kuwepo kwa mafuta feki ya kupaka aina ya Sunblock cream UV40 kwa ajili ya Albino yanayosaidia kujilinda dhidi ya saratani ya ngozi.Kulingana na Sanga mafuta feki ya albino yanauzwa kati ya sh.3500 hadi 6000 na mafuta halisi yanauzwa kati ya sh.40,000 hadi 90,000.
Taarifa imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa