SHIRIKA lisilo la kiserikali la TUSOME PAMOJA limetoa mafunzo ya siku moja kwa maafisa habari,maafisa elimu na wenyeviti wa waratibu Elimu kata katika Halmashauri zote nane za mkoa wa Ruvuma,mafunzo hayo yamefanyika kwa siku moja katika Hoteli ya Agapol Matogoro Manispaa ya Songea.
Mafunzo yaliyotolewa kwa maafisa hao yanahusu kuibua na kubadilishana simulizi za mabadiliko chanya katika maeneo yao ambapo wamekubaliana kuweka mpangokazi wa kufanya tafiti katika maeneo yao kwa kuangalia simulizi za mabadiliko chanya,kufanya mahojiano ya wahusika,kukusanya data,kuchambua na kuandika simulizi fupi kwa njia ya machapisho au video kisha kuziwasilisha TUSOME PAMOJA Mkoa wa Ruvuma Oktoba 9 mwaka huu.
Mratibu wa TUSOME PAMOJA katika Mkoa wa Ruvuma Steven Msabaha amesema simulizi za mabadiliko kutoka katika Halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma zinatarajiwa kuwasilishwa kimkoa kuanzia Oktoba 16 hadi 17 mwaka huu na kufanyiwa majadiliano ya wanahabari kupitia vyombo vya habari.
Uchunguzi umebaini kuwa simulizi za mabadiliko katika elimu zitasababisha shule nyingine kujifunza kutoka katika shule ambazo zimefanya vizuri na kufanya mabadiliko kwa kuiga au kubadilishana uzoefu wa masuala ya kielimu.
Akitoa historia ya shirika la TUSOME PAMOJA ambalo linafadhiliwa na USAID katika kipindi cha kuanzia Machi 2016 hadi Machi 2021,Mratibu wa TUSOME PAMOJA mkoani Ruvuma,Steven Msabaha amesema shirika hilo kwa sasa linafanyakazi katika mikoa minne ya Tanzania bara ambayo ni Ruvuma,Iringa,Mtwara na Morogoro pia linafanyakazi Tanzania Visiwani.
Msabaha amesema katika Mkoa wa Ruvuma TUSOME PAMOJA inafanyakazi katika Halmashauri zote nane za Mkoa zikiwa na jumla ya kata 173 na shule za msingi 766 na kwamba lengo la shirika hilo ni kushirikiana na serikali kupitia Wizara ya Elimu na TAMISEMI kuhakikisha kuwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo wanafunzi wa darasa la kwanza na pili waweze kusoma kwa ufasaha na kwamba hadi sasa TUSOME PAMOJA imetimiza miaka mitatu.
"Sera ya elimu ya mwaka 2014 imelenga kutoa elimu bora katika ngazi ya msingi na sekondari,Mkoa wa Ruvuma umeweka mkakati wa kuhakikisha hadi kufikia Novemba mwaka huu pasiwepo na mwanafunzi hata mmoja ambaye hajui kusoma,kuandika na kuhesabu,,katika kipindi cha miaka mitatu tumefanikiwa kuwajengea uwezo walimu karibu 570 wanaofundisha katika madarasa ya kwanza na pili,mafunzo ya uongozi kwa ngazi ya shule,kata,Halmashauri na Mkoa'',anasisitiza Msabaha.
Hata hivyo Msabaha amekiri kuwepo na udhaifu wa usimamizi katika shule na kata na kwamba kipimo cha elimu katika shule za msingi ni mitihani ya darasa la nne na la saba ambapo amesea mpango wa TUSOME PAMOJA ukisimamiwa vizuri katika shule za msingi hasa kuwatumia vizuri maafisa elimu wa kata unaweza kuleta mabadiliko chanya ndani ya muda mfupi ikiwemo kumaliza tatizo la wanafunzi kutojua kusoma na kuandika.
Amesisitiza kuwa maafisa elimu wa kata wanaweza kuzipitia shule katika kata zao kwa urahisi zaidi ukilinganisha na wadhibiti wa ubora wa elimu ambao hawawezi kupitia shule zote katika Halmashauri husika kutokana na mazingira ya kijiografia yaliopo.
Simulizi za mabadiliko zimelenga kukuza majadiliano na kujifunza zaidi kuhusu masuala ya kielimu yakiwemo yale yanayotekelezwa na Mpango wa TUSOME PAMOJA hali ambayo inagusa uigaji wa mambo mazuri yaliyofanywa na jamii nyingine ili kuboresha kiwango cha elimu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Septemba 12,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa