Jamii inatakiwa kujijengea utamaduni wa kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo ndani ya Manispaa ya Songea na kuvitangaza ili viweze kuvutia wawekezaji ndani ya mji wetu.
Kauli hiyo imetolewa na mtaalamu mwelekezi mkakati wa kuendeleza utalii Mkoa wa Ruvuma DR. H. Bohela Lunogelo katika kikao cha wakuu wa idara kilimo, mifugo, mipango, biashara, na maliasili kwa ajili ya kukusanya maoni na mkakati wa kuendeleza utalii kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea leo 13.10.2020.
Dr. Bohela Alisema ESRF ( economic and social research foundation) ni taasis inayofanya kazi ya utafiti wa kiuchumi na kijamii ambapo watafiti hao ni lazima wasimame mstari wa mbele na kutegemeana kwa ajili ya kushawishi viongozi, Serikali, na jamii kwa ujumla katika kuleta matokeo chanya ya uwekezaji katika vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya Manispaa ya Songea.
Nao wataalamu walioshiriki kikao hicho walisema “ pamoja na uwepo wa vivutio vingi vya kitalii Manispaa ya Songea lakini vivutio vifuatavyo vipewe kipaumbele ikiwemo na chanzo cha mto Ruvuma, Pango la asili la mlima chandamali, na Zoo Luhira ( hifadhi ndogo ya wanyama pori), kwa upande wa vivutio vya kiutamaduni wataalamu hao walipendekeza ngoma za asili, vyakula vya asili, Historia ya Chief Mbano, kwa upande wa vivutio vya kihistoria ni makumbusho ya Taifa ya majimaji, Mnara uliotumika kuwanyongea machief, pamoja na Makumbusho ya Mzee Kawawa.
Wakizitaja baadhi ya changamoto zinazokwamisha kutokuwa na vivutio bora vya kitalii ni pamoja na jamii kutofahamu uelewa wa umuhimu wa vivutio vya utalii, Mapungufu ya Sera kuhusu vivutio vya kitalii, na Miundombinu mibovu.
Pamoja na changamoto hizo, Manispaa ya Songea imeandaa mkakati wa kuboresha vivutio vya utalii ili wawekezaji waweze kuwekeza ndani Manispaa ya Songea.
IMETAYARISHWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
13.10.2020
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa