Na;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI;
MANISPAA YA SONGEA.
28/2/2022
Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. David Silinde (MB) amezitaka mamlaka za Serikali za mitaa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kutumia kumbukumbu na historia za Taifa kama chanzo cha ajira kwa wananchi ili kuchangia katika mapambano dhidi ya umaskini nchini.
Amebainisha hayo katika tamasha la kumbukizi ya miaka 115 ya vita vya Majimaji na utalii wa utamaduni iliyofanyika hapo jana tarehe 27 februari 2022 katika eneo la Makumbusho ya Taifa ya vita vya Majimaji lililopo Mtaa wa Mashujaa ndani ya Manispaa ya Songea, tukio ambalo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Silinde alisema kuwa njia bora ya kuwaenzi mashujaa wa vita vya Majimaji ni pamoja na kuhifadhi utamaduni kwa kufanya kazi kwa bidii, kulinda rasilimali za Taifa, kupambana na kuzuia rushwa, ujangili na maatumizi ya madawa ya kulevya kwa kutunza maadili ya mila na desturi za kale kupitia kizazi hadi kizazi. ’Alisisitiza’
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Pololet Kamando Mgema ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Songea amewataka wananchi wa Ruvuma kuiga uzalendo wa mashujaa hao kwa kudumisha Amani, mshikamano na umoja kwa kuzingatia misingi ya utamaduni iliyowekwa na mashujaa wa vita vya Majimaji.
Ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano katika zoezi la utoaji Anwani za makazi na postikodi pamoja na sensa kwa lengo la kuisadia Serikali katika upangaji mikakati ya maendeleo kwa wannachi wake.
Naye mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Ezekiel Mwakalukwa alieleza kuwa Tamasha hilo hufanyika kila mwaka kuanzia tarehe 25 hadi 27 februari kwa lengo la kuwakumbuka mashujaa waliopigana vita vya Majimaji ambapo mashujaa 67 walinyongwa na wakoloni wa Ujerumani mnamo Februari 27 mwaka 1906 na kuzikwa katika makubiri yaliyopo ndani ya makumbusho ya Taifa ya vita vya Majimaji, pamoja na kuinua utalii wa utamaduni nchini Tanzania.
Ametoa rai kwa wadau na wanachi wote kwa ujumla kuendeleza uzalendo pamoja na kuona fursa na kiuchumi zilizopo kupitia utalii wa utamaduni.
Kauli mbiu katika Tamasha hilo ni “Utamaduni wetu, nguvu yetu kwa maendeleo ya Utalii wa uchumi”.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa