TUKIWA katika wiki ya mazingira duniani,uchomaji moto hovyo misitu ya hifadhi na maeneo yaliohifadhiwa kisheria umekuwa unaleta athari za kimazingira katika maeneo mbalimbali nchini.
Kila mwaka majira ya kiangazi kuna kesi nyingi za uchomaji moto hovyo misitu na mapori ambao unasababisha hasara kubwa kiuchumi lakini pia kuathiri viumbehai wanaoishi katika maeneo hayo.
Kwa mfano mara kadhaa msitu wa serikali wa SAO HILL wenye urefu wa kilometa 60 uliopo Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa kumekuwa na matukio ya kuchomwa moto.
Msitu huo unapoteketezwa na moto unaleta athari kubwa kimazingira kwa kuwa SAO HILL ni miongoni mwa chanzo cha mto Ruaha mkuu ambao ni muhimu sana kwa viumbehai na uchumi wa Tanzania.
Wataalam wa mazingira wanaonya kuwa msitu wa SAO HILL ukiteketea wote kwa moto unaweza kusababisha hasara kubwa kwa serikali kwa kuwa gharama kubwa ilitumika na serikali kuanzisha msitu huo katika kipindi cha awamu ya kwanza cha hayati Baba wa Taifa mwalimu Julius Nyerere kwa kuwa serikali ilikopa Benki ya Dunia miaka ya 60 mamilioni ya dola za kimarekani kwa ajili ya kuanzisha msitu huo.
Uchunguzi unaonesha kuwa msitu wa SAO HILL ni moja ya mapafu ya Tanzania kwa kuwa iwapo itakauka kwa kuchomwa inaweza kusababisha chanzo cha maji cha mto Ruaha kilichopo katika msitu huo kuathirika hivyo Tanzania inaweza kugeuka jangwa.
Ukiachia msitu wa SAO HILL,Uchomaji moto hovyo pia umekuwa unatokea katika msitu wa serikali wa Matogoro uliopo Manispaa ya Songea na pori la akiba la wanyama la Liparamba wilayani Mbinga na kuathiri pori hilo ambalo lipo mpakani na nchi yetu na nchi ya Msumbiji.
Kulingana na uchunguzi,mikoa yote nchini yenye misitu aina ya miyombo, ina matukio mengi ya moto. Mikoa hiyo ni Rukwa, Mbeya, Tabora, Kigoma, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Morogoro na Pwani.
Uchunguzi pia umebaini kuwa Kutokana na moto kuvuka mipaka ya mikoa bila kujali ulianzia wapi ni vigumu kubaini mkoa gani unaongoza kwa uchomaji moto katika Tanzania.
Hata hivyo ripoti ya Wizara ya Mazingira inataja utekelezaji wa Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji, ambapo Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji, kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii,inaendeleza mikakati ambayo inalenga kudhibiti uchomaji moto.
Sera ya Taifa ya misitu inaelekeza wananchi kuhifadhi na kuendeleza misitu kwa njia ya usimamizi shirikishi wa misitu.
Sheria ya usimamizi wa mazingira namba 20 ya mwaka 2004 fungu namba 187 kwa makosa yanayohusu uchafuzi wa mazingira ya maji, hewa, ardhi na uchomaji misitu hovyo inaagiza kuwa mtu yeyote atakayekiuka chochote cha sheria hiyo akitiwa hatiani atatozwa faini isiyozidi milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka saba jela ama vyote viwili.
Wiki ya mazingira duniani huadhimishwa kila mwaka kuanzia Mei 31 na kilele chake Juni 5,ambapo mwaka huu katika mkoa wa Ruvuma maadhimisho hayo yanafanyika Kata ya Mjimwema Manispaa ya Songea,mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme.
Makala hii imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 2,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa