UFAULU wa wanafunzi kwa kidato cha nne katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma umetoka asilimia 73.2 mwaka 2016 na kufikia asilimia 88 mwaka 2017. Hata hivyo katika mwaka 2017/2018 jumla ya wanafunzi 19 walibainika na kuripotiwa kuwa na mimba.
Halmashauri ina jumla ya Shule za Sekondari 40, kati ya hizo 24 zinamilikiwa na serikali na 16 za binafsi. Jumla ya wanafunzi katika shule za sekondari za Serikali ni 12,404 ikiwa Wavulana ni 5,893 na Wasichana ni 6,511 na wale wa Shule binafsi ni 4,536, Wavulana 2,438 na Wasichana ni 2,098.
Hata hivyo Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina Shule tano zenye wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita ambazo zina jumla ya Wanafunzi 2,146 ikiwa Wanafunzi 992 ni Wavulana na Wanafunzi 1,154 ni Wasichana.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea imeendelea kutengeneza madawati kwa kutumia karakana yake ambapo tayari hivi sasa madawati 160 yametengenezwa kwa ajili ya kupelekwa kwenye Shule za Sekondari. Pia Halmashauri inaendelea kutengeneza madawati katika karakana yenye thamani ya Tshs. 26,000,000.00.
Katika mwaka 2018/2019 Halmashauri ya Manispaa ya Songea inatarajia kupokea kiasi cha Tshs. 325,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni matatu yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80 kila bweni na madarasa matano pamoja na meza 40 na viti 40 katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea.
Halmashauri pia imepokea fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi katika Shule za sekondari kupitia mpango wa Lipa kulingana na Matokeo (P4R). Kupitia mpango huo Halmashauri Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 imepokea jumla ya Tsh. 17,000,000/= ambazo zimetumika kwa ukamilishaji wa vyumba viwili vya maabara na matundu tisa ya choo katika Shule mbili za sekondari za Lukala na Londoni.
Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ya Manispaa ya Songea imepokea jumla ya Tsh 162,700,000/= kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba 14 vya maabara katika shule za sekondari 8 na kaazi imekamilika kwa asilimia 90% na kunufaisha wanafunzi wapatao 5972.
Kuhusu fedha za elimu bila malipo,manispaa ya Songea Kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo 2016/2017 na 2017/2018, kupitia Mpango wa Elimu bila malipo Halmashauri imepokea jumla ya Tshs. 2,887,986,760.00,ambapo Upatikanaji wa fedha hizo umeboresha miundombinu ya madarasa, vyoo, samani, upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia shuleni na hivyo kufanya kazi ya ufundishaji kuwa rahisi kwa Walimu sawa na asilimia 100 ya utekelezaji wa fedha zilizopokelewa za Elimu Bila malipo.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Septemba 19,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa