Afisa wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Frank Komakoma alisema lengo la serikali ni kuhakikisha zoezi hili la ugawaji wa dawa linatekelezwa vizuri ili kila mtoto/mwanafunzi aweze kupewa dawa hizo.
Komakoma alitamka hayo akiwa katika mafunzo kwa walimu wakuu wa shule za msingi 91, waratibu elimu kata 21, walimu wa afya, na wataalamu Sekta ya elimu kwa ajili ya kuwaandaa katika kusimamia zoezi la ugawaji wa dawa za minyoo ya tumbo na kichocho kwa wanafunzi 58,000 wenye umri wa miaka 5-14 linalotarajia kufanyika kuanzia 18.09 hadi 21.09.2020 Manispaa ya Songea.
Alisema Wizara ya Afya imeweka malengo mkakati ya utekelezaji wa mpango wa kuongeza upatikanaji wa huduma, tiba na kujenga uwezo wa utekelezaji wa mpango huu kwa jamii ili jamii iwe na afya bora.
Naye Mratibu wa kanda ya Chabruma Manispaa ya Songea dr. Stephen Chacha alisema “ magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ni magonjwa ambayo yamo ndani ya jamii maskini lakini jamii yenyewe na hata wataalam husika ama viongozi hawayapi umuhimu kulingana na madhara yake katika jamii. Akiyataja magonjwa hayo ni usubi, Matende na mabusha, Trakoma, kichocho na minyoo ya tumbo.”
Dr. Chacha alisema kichocho husababishwa na minyoo inyoitwa jamii ya Schistosoma ambao unaenezwa na konokono kwa kutoa vimelea kupitia maji yaliyotuama.
Alisema kichocho husababisha damu kutoka kwenye njia ya mkojo na choo, na baadae inaweza kusababisha saratani ya tumbo, kibofu cha mkojo na ini.
Aliongeza kuwa minyoo ya tumbo imegawanyika katika aina tatu 3 nayo ni minyoo mviringo, minyoo mjeledi, na minyoo ya safura ambayo huishi kwenye udongo na husababisha mtu kuwa dhaifu na kuishiwa damu na isipotibiwa mapema inaweza kusababisha utumbo kujifunga na kifafa, pia inaweza kumfanya mtoto ashindwe kuhudhuria shule au kutoelewa vizuri.
Alizitaja njia za kujikinga na magonjwa hayo ni pamoja na kutumia dawa za kutibu na kudhibiti magonjwa haya ambazo hutolewa kila mwaka kwa jamii iliyoathirika, kuzingatia usafi wa uso na mwili, usafi wa mazingira, kutokuoga kwenye maji yasiyo safi na yaliyotuama (bwawa), kujikinga kuumwa na inzi au mbu, na kutoa elimu ya afya ya jamii.
Alisema kwa ugonjwa wa kichocho unatakiwa kumeza dawa ya praziquantel kwa miaka mitano mfululizo, ugonjwa wa minyoo ya tumbo na usubi na matende hutumika katika kujikinga na kutibu kwa dawa ya Mectizan na Albendazole, ugonjwa wa trakoma hutumia kutibu dawa ya Zithromax.
Aidha, imefafanuliwa kuwa mwalimu amepewa moja ya majukumu ya kutoa elimu ya afya kuhusu manufaa na maelekezo ya umezaji dawa husika kwa kiongozi wa shule, wazazi, na wanafunzi, kuandikishwa walengwa (wanafunzi) kwenye rejista, kuaandaa chakula kwa ajili ya wanafunzi kabla ya kumeza dawa na Dawa hiyo imezwe ndani ya masaa mawili baada ya kula chakula.
Naye afisa elimu Manispaa ya Songea Zakia Fandey amesema atahakikisha anasimamia vizuri shule zote na atahakikisha kila mtoto aliyeandikishwa shule anapewa dawa hizo.
IMETAYARISHWA NA;
AMINA Y. PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
17.09.2020
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa