UJENZI wa barabara ya lami nzito kutoka Mbinga hadi Mbambabay Makao Makuu ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma,umeanza rasmi.Kampuni ya China Henan International Corparation Group Ltd (CHICO) ambayo imeingia mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo na serikali,tayari imepeleka mitambo mbalimbali ya kisasa ya ujenzi wa barabara hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa na Naibu Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhandisi Stella Manyanya ametembelea eneo ambalo Kampuni hiyo inakamilisha kambi lao ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mwisho ya ujenzi wa kambi.
Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 67 toka Mbinga hadi Mbambabay ambayo itagharimu shilingi bilioni 129.
Mkataba huo wa miezi 24 umesainiwa Desemba 11,2017 na Kampuni ya CHICO ambayo inatarajia kukamilisha kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2020.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa,Mhandisi Manyanya amesema kukamilika kwa barabara hiyo kunafungua milango ya utalii katika mwambao mwa ziwa Nyasa ambako kuna karibu aina zote za vivutio vya utalii na uwekezaji na kwamba barabara hiyo itakuwa kiungo muhimu cha nchi za Tanzania,Malawi na Msumbiji ambazo zitatumia bandari ya Mbambabay.
Kukamilika kwa kipande cha barabara toka Mbinga hadi Mbambabay kunakamilisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami katika ukanda wa Mtwara Corridor toka Mtwara hadi Mbambabay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma hivyo kufungua milango ya uwekezaji na utalii katika ukanda wa kusini.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 19,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa