TAFORI kuhusu ukweli wa miti ya kigeni na matumizi ya maji imebainisha kuwa mwaka 2000 eneo la mashamba ya miti ya kigeni aina ya mikaratusi duniani kote lilikaribia hekta milioni 18 kati ya hizo asilimia 37 ya eneo hilo lilikuwa barani Afrika na asilimia 73 ya eneo hilo lipo Afrika ya kusini. MITI aina ya mikaratusi inadaiwa inaongoza kwa kunyonya kiwango kikubwa cha maji ardhini hali ambayo inachangia kuharibu vyanzo vya maji pale inapopandwa jirani na vyanzo hivyo.
Kuna taarifa kuwa mti mmoja mkubwa wa mkaratusi una uwezo wa kunyonya maji kiasi cha milimita 300 kwa siku kutoka ardhini hivyo katika maeneo mengi vyanzo vya maji ambayo imepandwa miti hiyo inadaiwa imeua vyanzo vya maji na kusababisha ukame.
Kwa mfano katika msitu wa serikali uliopo milima ya Matogoro nje kidogo ya mji wa Songea ,imepandwa miti aina ya mikaratusi ambayo inatajwa kuchangia kuharibu vyanzo vya maji vilivyopo katika milima hiyo ambavyo ni muhimu kwa kuwa vinatumika kusambaza maji yanayotumiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Taka Songea SOUWASA kusambaza maji katika manispaa ya Songea.
Pia katika msitu wa mlima Matogoro kuna chanzo cha mto Ruvuma ambao ni maarufu kwa kuwa ni miongoni mwa mito mikubwa Tanzania ambao unamwaga maji yake Bahari ya Hindi.Mto huo pia unatenganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji.
Kutokana na hali hiyo serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii iliamuru miti yote aina ya mikaratusi katika msitu wa serikali wa Matogoro kuvunwa kwa wakati mmoja ili kuepuka ukame na kupanda miti ya asili inayokua polepole ambayo ni rafiki katika vyanzo vya maji.
Hata hivyo Utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa sio miti yote aina ya mikaratusi ikiwemo ya milima ya Matogoro ina tabia ya kunyonya maji kwenye vyanzo vya maji.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu nchini (TAFORI) unaonesha kuwa kuna aina ya miti ya mikaratusi ambayo ni rafiki wa vyanzo vya maji ndiyo maana katika misitu mingine nchini kama ile ya Sao Hill Mafinga Mkoa wa Iringa imepandwa miti ya mikaratusi tena karibu na vyanzo vya maji ambavyo vimeendelea kutoa maji na hakuna dalili zozote za ukame au maji kupungua.
TAFORI pia imebaini kuwepo kwa aina kadhaa ya miti aina ya mikaratusi ambayo kwa kiwango kikubwa inanyonya maji mengi.
Kulingana na utafiti wa TAFORI miti hiyo ni Mikaratusi jamii ya Camaldulensis ambayo hunyonya maji kiasi cha milimita 1,240 kwa mwaka na Mikaratusi aina ya Microrhea inayonyonya maji milimita 1,050 kwa mwaka, Mikaratusi ya aina ya Patula nayo hunyonya maji kiasi cha milimita 665 kwa mwaka.
Changamoto iliyopo hivi sasa ni kwamba miti mingi aina ya mikaratusi imekwishaondolewa isipokuwa tatizo la kujiotea kila inapovunwa ndilo linalosumbua na kuathiri miti ya asili ambayo imepandwa.
Taarifa ya TAFORI inabainisha kuwa mashamba mengine makubwa ya mikaratusi barani Afrika yapo katika nchi za Morocco,Angola,Ethiopia na Tunisia na kwamba katika Afrika mashariki nchi ya Kenya inaongoza kwa mikaratusi ikifuatiwa na Uganda na Tanzania na kwamba maeneo ya mikaratusi katika nchi za Burundi na Rwanda ni maradufu ya maeneo ya nchi ya Kenya.
Kutokana na utafiti huo TAFORI inabainisha kuwa Tanzania haijumuishi kwenye nchi maarufu kwa upandaji wa mikaratusi na kwamba haiwezi kuchukua nafasi ya kwanza kubaini madhara ya mikaratusi.
Hata hivyo utafiti ambao umetolewa na TAFORI kuhusu miti ya kigeni na matumizi ya maji unaonesha kuwa mikaratusi iliyopo katika nchi ya Sudan kwa mwaka matumizi yake ya maji ni milimita 1240 wakati mikaratusi katika nchi ya Pakstani matumizi ya maji kwa mwaka ni milimita 1500.
Utafiti huo unaonesha kuwa mikaratusi iliyopo nchini Kenya kwa mwaka matumizi ya maji ni milimita 830 na miti aina ya misindano Tanzania katika msitu wa Sao hill Mafinga kwa mwaka hutumia maji milimita 665.
Kulingana na utafiti huo matumizi ya maji kwa mwaka kwa miti mingine na mazao ukilinganisha na mikaratusi unaonesha kuwa miti aina ya mvinje iliyopandwa Bura nchini Kenya kwa mwaka inatumia maji milimita 5437, jamii ya mpingo katika eneo la Bura Kenya kwa mwaka inatumia maji milimita 1143 na Mgunga nchini Paktan unatumia milimita 2100 za maji kwa mwaka.
Utafiti huo unaonesha kuwa mazao ya kilimo nchini Pakstani yakiwemo ngano kwa mwaka yanatumia milimita 330 za maji,pamba milimita 460,mahindi nchini Marekani kwa mwaka yanatumia maji milimita 630 na pamba ya Marekani inatumia maji milimita 630.
Zao la korosho hapa nchini katika Wilaya ya Nachingwea kwa mwaka linatumia maji milimita kati ya 814 hadi 1409,mpunga nchini Pakstan kwa mwaka unatumia maji milimita 1620 na miwa katika nchi ya Pakstani inatumia maji milimita 1400 kwa mwaka.
Utafiti huo unaonesha kuna miti kama mvinje na mgunga inatumia maji mengi kuliko mkaratusi na kwamba yapo baadhi ya mazao kama mpunga na miwa ambayo yanatumia maji karibu sawa au zaidi ya mikaratusi.
Miaka ya karibuni Wizara ya Maliasili na Utalii, baadhi ya viongozi,na wadau wa mazingira wameilaumu mikaratusi(eucalyptus) iliyopandwa katika Msitu wa Serikali Matogoro Wilaya ya Songea kutokana na kudaiwa miti hiyo inanyonya maji katika kiwango kikubwa na kutishia vyanzo vya maji vilivyopo katika msitu huo.
Kutokana na hali hiyo yalifanyika maazimio ya kuing’oa miti hiyo kwenye msitu wa serikali wa milima ya Matogoro na kupanda miti ya asili .
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa