MKUU wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma,Pololet Mgema amekagua Ujenzi wa Kituo cha kupooza Umeme kilichopo Unangwa Manispaa ya Songea na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa kituo hicho
Mgema amesema serikali imedhamiria kuhakikisha Mkoa wa Ruvuma unaunganishwa na umeme wa Grid ya Taifa kutokea Makambako hadi mjini Songea kupitia Madaba.
Juni 24 mwaka huu TANESCO ilizima njia ya kusafirishia umeme ya 220k Mufindi-Mbeya ili kuruhusu mafundi kuingiza umeme katika kituo kipya cha Madaba mkoani Ruvuma.
Kituo cha kupoozea Umeme cha Unangwa mjini Songea ni moja kati ya vituo vitatu vya kupooza umeme wa msongo mkubwa wa 220kv kabla ya kuupeleka kwa watumiaji.
Vituo vingine vya kupoozea umeme ni Madaba Wilayani Songea na Makambako Mkoani Njombe.
Taarifa ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) inaonesha kuwa njia kuu ya kusafirisha Umeme wa Msongo Mkubwa kutoka Makambako umekamilika kwa asilimia kubwa na kwamba kazi zilizobaki ni ukamilishaji wa vituo hivyo vya kupoozea umeme.
Kulingana na TANESCO umeme wa Grid ya Taifa unatarajiwa kuwashwa mjini Songea Septemba mwaka huu na kazi ya kusambazwa kwa watumiaji inaendelea kufanywa na Shirika hilo.
Tangu mwaka 2016 tatizo la mgawo wa umeme katika mji wa Songea limebakia kuwa historia mara baada ya TANESCO Ruvuma kuanza kununua umeme wa maji kutoka Tulila mto Ruvuma.
Chanzo hicho cha maji kinamilikiwa na Watawa Wabenediktine wa Mtakatifu Agnes Chipole Jimbo Kuu Katoliki la Songea ambapo hadi sasa wana mashine mbili zenye uwezo wa kuzalisha megawati tano,lengo ni kuzalisha umeme megawati 7.5.
Mahitaji ya umeme katika mji wa Songea ni kilowatts 4300 hivyo basi kutokana na umeme wa maji unaozalishwa Tulila,TANESCO Ruvuma imefanikiwa kumaliza kabisa tatizo la mgawo wa umeme katika mji wa Songea.
TANESCO Ruvuma hivi sasa inatumia umeme wa Tulila katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea,Halmashauri ya Wilaya ya Songea,Mbinga na Nyasa.
Baada ya kukamilika kwa mradi huu mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta mazito hapa Songea, Madaba na Mbinga itazimwa na kupelekea kuokoa gharama kubwa zinazotumika na TANESCO kuzalisha umeme.
Mkuu wa Wilaya ya Songea anawakaribisha Wawekezaji Wazawa na Wageni kuwekeza katika wilaya hiyo Songea kuwekeza katika ujenzi wa viwanda kwa sababu sasa wilaya ya Songea itakuwa na umeme wa kutosha,uhakika na kuaminika.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 25,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa