HATIMAYE umeme wa Gridi ya Taifa umefika mjini Songea na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kupitia Makambako na Madaba. Mashine za Mafuta (Diesel Generetors) za Madaba zimezimwa rasmi na wananchi wanafurahia umeme wa Gridi.Tayari Wizara ya Nishati kupitia TANESCO imewaangazia maisha Wananchi wa mkoa wa Ruvuma.
Hata hivyo Waziri wa Nishati Dkt.Merdad Kaleman amesema Ifikapo Septemba 26 mwaka huu itawashwa mitambo yote na wananchi wataanza rasmi kutumia umeme kutoka kwenye mradi huu wa Makambako-Songea“Tukiwasha mitambo ya mradi huu tutazima rasmi mitambo ya umeme iliyokuwa inatumia mafuta mazito iliyoko Madaba, Ludewa, Mbinga, Namtumbo na Songea Mjini’’,anasisitiza Waziri wa Nishati.
Serikali imejenga mradi mkubwa wa kusafirisha umeme wa Grid ya Taifa kutoka Makambako mkoani Njombe,kupitia Madaba hadi Songea mjini umbali wa kilometa 250 ili umeme wa kutosha uweze kuwafikia wananchi na utumike kwa maendeleo endelevu.
Serikali imejenga vituo vya kupoozea umeme huo wa Grid ya Taifa na kuuongeza nguvu kutoka kilovolti 132 hadi kilovolti 220 ambao utakuwa umeme mkubwa kwa matumizi ya viwanda.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa umeme wa REA mkoani Ruvuma,Waziri wa Nishati Dkt.Merdad Kalemani aliahidi kuwa umeme wa Grid ya Taifa utawashwa mjini Songea Septemba 2018 jambalo liliahidiwa na limetekelezwa kwa wakati.
Waziri Dkt.Kalemani alisisitiza kuwa umeme huo wa Grid ya Taifa pia utatumika kusambaza umeme katika vijiji 120 vya mkoa wa Ruvuma na Njombe na kwamba umeme huo utatoa umeme kwa wateja wapya 22,700.
Kulingana na Waziri Kalemani, umeme huo utasambazwa katika wilaya zote za mkoa wa Ruvuma na wilaya za Ludewa na Njombe mkoani Njombe umbali wa kilometa 900 hivyo kuwezesha sasa mkoa wa Ruvuma kuanza kupata umeme wa uhakika na kuaminika hivyo kufungua fursa za uchumi wa viwanda.
Waziri Kalemani anawashauri watanzania kutumia umeme kwa kujenga viwanda vidogo na kusindika mazao mbalimbali ambayo yanalimwa katika mkoa wa Ruvuma yakiwemo Mahindi, Kahawa,korosho,alizeti na mazao ya matunda ili kuongeza thamani ya mazao wanayozalisha.
Sera ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanapata nishati ya umeme,ambapo takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watu wanaopata nishati ya umeme nchini imepanda toka asilimia 10 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 67 mwaka 2017.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari serikalini
Septemba 14,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa