UTAFITI umeonesha kuwa, asilimia zaidi ya 96 ya chembe za urithi za binadamu zinafanana na zile za sokwe, pia ubongo wa sokwe na vitendo vyao vinafanana sana na vile vya binadamu.
Profesa Richard wa somo la viumbe kutoka Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani anaeleza kuwa, sokwe ni daraja pekee kati ya binadamu na maumbile hivyo ni vema wanyama hao kulindwa kwa nguvu zote.
Mhifadhi wa Hifadhi za Taifa,Noelia Mnyonga anasisitiza tafiti za kisayansi zimethibitisha kuwa Sokwe ni wanyama ambao wanafanana na binadamu katika tabia kwa asilimia 98 na kusisitiza kuwa ndiyo maana wanaitwa sokwe mtu.
“Sokwemtu ni mnyama ambaye alibakiza asilimia mbili tu angeweza kufanana na binadamu kitabia kwa asilimia 100 hali ambayo inamfanya mnyama huyu kutafutwa kwa udi na uvumba baada ya kuwa kivutio adimu na cha kipekee cha utalii duniani kote’’,anasema Mnyonga.
Mnyonga anasisitiza kuwa sokwe mtu ni mnyama wa ajabu ambaye kwa tabia na matendo hatofautiani sana na binadamu ndiyo maana baadhi ya watu wanamuita binadamu pori.
Sokwe mtu ni mnyama ambaye ni mfano halisi wa binadamu, mnyama huyu anavutia macho ya watalii wengi,ambao wanamiminika hapa nchini katika hifadhi ya Taifa ya Gombe kwenda kuwashangaa wanyama hao adimu na wa aina yake.
Tafiti za kisanyansi zinaonesha kuwa sehemu ya ubongo wa sokwe inafanana na sehemu ya ubongo wa binadamu,hali hiyo ndiyo imesababisha sokwemtu kufanya matendo mengi ambayo yanafanywa na binadamu kwa mfano sokwemtu anaweza kupiga mswaki,kula chakula na kucheza kama binadamu.
“Sokwe anaweza kufanya mambo mengi kama anavyofanya binadamu, hali hiyo imewavutia watalii na watafiti wa kimataifa kufika katika hifadhi ya Taifa ya Gombe kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tabia za wanyama hawa”,anasema mhifadhi Mnyonga.
Hifadhi ya Taifa ya Gombe ilipata umaarufu duniani baada ya mtafiti wa tabia za sokwe duniani Dk.Jane Gooddall raia wa nchi ya Uingereza kufanya utafiti kuhusu maisha na tabia ya sokwe wa Gombe kwa muda wa miaka 40 na kuandika vitabu kadhaa kuhusu wanyama hao.
Dk.Goodall ndiye alitoa tahadhari ya kuhakikisha kuwa wanyama hao walio na ukoo wa karibu na mwanadamu hawaangamii kabisa na kuonya iwapo hatua za makusudi hazitachukuliwa za kuwalinda, sokwe wanaweza kuangamia.
Mwanasayansi Dk.Gooddall anasema katika nusu karne iliyopita, idadi ya sokwe ilipungua kutoka takribani milioni mbili hadi kufikia laki tatu pekee katika nchi 21, ambapo hivi sasa hali ni mbaya zaidi kutokana na aina adimu ya sokwe wamesalia Tanzania pekee.
Tanzania ina Hifadhi za Taifa 16 ambazo ni hifadhi ya Taifa Arusha,Gombe,Katavi,mlima Kilimanjaro, Mahale, Mikumi, Ziwa Manyara,Ruaha,Rubondo, Serengeti, Saadan, Tarangire, Udzungwa,Kitulo, Mkomazi na Saanane.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 18,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa