GHARAMA za utafutaji mafuta na gesi asilia hutofautiana kulingana na hatua ambayo imefikiwa na mwekezaji na eneo la utafutaji. Kwa mfano, utafutaji mafuta baharini kwenye maji ya kina kirefu hugharimu fedha nyingi kiasi cha takriban shilingi bilioni 100 kwa kuchimba kisima kimoja ikilinganishwa na utafutaji nchi kavu ambao unagharimu kiasi cha takriban sh. bilioni 25.
Bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Kinyerezi Dar es salaam limekamilika ambapo bomba la gesi lenye ukubwa wa milimita 36 limezamishwa ardhini na kwa mujibu wa wataalam linaweza kuishi hadi miaka 400.
Hata hivyo mtambo uliotumika kufunga mabomba ndani ya bahari umekodiwa kwa gharama kubwa ambapo kwa siku moja mwenye mtambo huo analipwa sh. bilioni tatu na kwamba mtambo huo umekaa baharini miaka miwili ukiwa na wafanyakazi 300 umbali wa kilometa 200 ndani ya bahari kutoka Mtwara.
Kutokana na ukubwa wa gharama hizo, Serikali inaingia mikataba na wawekezaji ambapo rasilimali inabaki kuwa ni mali ya Taifa. Serikali haina gharama wakati wa utafutaji na mgao hufuatana na mfumo wa ugawanaji (production sharing).
Hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuhamasisha uwekezaji ni pamoja na uwepo wa Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji Mafuta inayosimamia shughuli zote za utafutaji na uzalishaji mafuta na gesi, Mikataba ya Ugawanaji inayosimamiwa na TPDC kwa niaba ya Serikali na Sera ya Gesi Asilia.
Katika kuongeza uwekezaji zaidi, Serikali kwa hivi sasa imetayarisha Sera ya Mafuta, Sera ya Uwezeshaji Wananchi katika miradi ya Mafuta na Sheria ya Gesi Asilia.
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imetekeleza mradi wa ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asilia katika maeneo ya Madimba Wilaya ya Mtwara Vijijini na Songo Songo Wilayani Kilwa na bomba la kusafirishia gesi asilia kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es salaam kupitia Somanga Fungu. Mradi huu ulikamilika Desemba, 2014.
Mitambo ya kusafisha gesi asilia iliyopo Madimba ina uwezo wa kusafisha gesi asilia kiasi cha futi za ujazo milioni 210 kwa siku na mitambo ya Songo Songo futi za ujazo milioni 140 kwa siku. Bomba la kusafirisha gesi asilia lina urefu wa kilomita 542.
Katika hali ya kawaida ya uendeshaji, bomba hili ambalo linaweza kuishi miaka 400, litakuwa na uwezo wa kusafirisha kiasi cha futi za ujazo milioni 784 kwa siku. Uwezo huu unaweza kuongezeka mpaka futi za ujazo milioni 1,002 kwa siku kwa kufunga mitambo ya kuongeza msukumo wa gesi asilia.
Mradi huu unaunganisha maeneo yanayozalisha gesi asilia hususan Mnazi Bay, Songo Songo, Kiliwani, Mkuranga, Ntorya na gesi iliyogunduliwa katika eneo la bahari ya kina kirefu. Vile vile, bomba lina matoleo maeneo ya Mtwara, Lindi, Kilwa, Somanga Fungu na Mkuranga kwa ajili ya matumizi ya gesi asilia katika maeneo hayo.
Mwandishi wa makala haya ni Albano Midelo
Mawasiliano albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa