UZALISHAJI wa zao la korosho katika Mkoa wa Ruvuma umeongezeka kutoka tani 8,502 msimu wa mwaka 2015/2016 hadi kufikia tani 21,500 msimu wa mwaka 2017/2018.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015 katika kipindi cha Julai 2017 hadi Juni 2018,kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 152.
Mndeme amebainisha kuwa ongezeko hilo limeenda sanjari na kipato cha mkulima ambapo bei ya juu ya kilo moja ya korosho katika mnada kwa msimu wa mwaka 2016/2017 ilifikia kiasi cha shilingi 4010.00 na kwamba bei hiyo haijawahi kufikiwa katika msimu wowote wa uzalishaji.
“Malengo ya uzalishaji wa zao hilo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2018/2019 kuwa ni kufikia tani 30,000’’,anasisitiza Mndeme.
Akizungumzia uzalishaji wa zao la kahawa,Mkuu huyo wa Mkoa wa Ruvuma amesema zao hilo pia uzalishaji umeongezeka kutoka tani tani 12,488 msimu wa mwaka 2015/2016 hadi kufikia tani 17,223 msimu wa mwaka 2017/2018 sawa na ongezeko la asilimia 38.
Hata hivyo amesema kumekuwepo na jitihada za kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la kahawa na kwamba Mkoa wa Ruvuma unaye Mwekezaji mkubwa wa zao la kahawa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea kijiji cha Lipokela anayeitwa AVIV ambaye anazalisha wastani wa tani 1400 katika eneo la hekta 1,036.
Mkoa wa Ruvuma unaendelea na jitihada za kuboresha mazao makuu ya kimkakati yanayolimwa ambayo ni kahawa,korosho na tumbaku ambayo uzalishaji wake umekuwa ni wa kuridhisha.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini
Septemba 7,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa