VIJANA 153 katika Mkoa wa Ruvuma wanatarajia kupata mafunzo ya ujasiriamali na biashara kwa viajana yanayotolewa na Baraza la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC).
Akitoa taarifa katika ufunguzi wa mafunzo awali ya ujasiriamali kwa vijana 50 kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea, Mwakilishi wa NEEC Silas Daudi alisema katika mafunzo hayo jumla ya vijana 153 wanatarajia kupata mafunzo hayo ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi Taifa.
Alisema mafunzo hayo ni sehemu ya program ya Ujasiriamali kwa vijana wenye umri kati ya miaka 18 -35 katika mikoa ya Tanzania Bara yenye lengo la kuwezesha na kuboresha mbinu za uendeshaji na usimamizi wa biashara na urasimishaji wa shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa na vijana.
Daudi aliyataja malengo mengine ya mafunzo hayo kuwa ni kuwawezesha vijana wanaomiliki biashara katika mkoa husika kukuza na kurasimisha biashara zao ili kuongeza ajira kwa vijana wenzao na kuchangia kikamilifu katika pato la taifa.
Kwa mujibu wa Mwakilishi na NEEC, mafunzo hayo yatafanyika katika mikoa nane,ukiwemo Mkoa wa Dodoma ambako mafunzo yameshafanyika kwa vijana 204 na kwamba katika Mkoa wa Ruvuma ambako mafunzo yanafanyika sasa.
Ameitaja mikoa mingine ambayo mafunzo hayo yatafanyika kuwa ni Geita, Mwanza, Lindi, Mbeya, Tanga na Arusha.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ( NEEC) Beng’i Issa alisema NEEC inasimamia programu ya mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana kujiajiri ambayo hivi sasa inatekelezwa katika mikoa mitano.Lengo likuwa ni kuchukua vijana ambao hawajasoma na wanaotoka katika familia masikini.
“Kupitia program hii vijana wanapata mafunzo kwa vitendo,wanafuatiliwa,na wanapewa wafanyabiashara wenye uzoefu kuwatembelea kwa muda wa mwaka mmoja.” alisisitiza Issa.
Katibu Mtendaji huyo alisema wametoa muongozo wa kufundisha somo la ujasiriamali katika shule za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu.
Naye mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa Ruvuma Hakimu Mafuru ameiomba serikali kutunga vitabu ambavyo vinaelezea mada za ujasiriamali ili kuwajengea uwezo vijana.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Phillip Benno, alisema Halmashauri imejipanga kuwa kutumia asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kuwawezesha vijana.
Programu ya mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana inatarajia kuwanufaisha vijana 40,000 katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Imeandikwa na Farida Mussa
Wa Kitengo cha TEHAMA Manispaa ya Songea
Agosti 10,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa