JUMLA ya vijana 55 wamehitimu kozi ya miezi mitatu ya Askari wanyamapori vijijini(VGS) katika chuo cha Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii(CBCTC) kilichopo Likuyu Sekamaganga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo namba 63 ya mwaka 2018 alikuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Generali Gaudence Milanzi.Akizungumza katika mahafali hayo Katibu Mkuu huyo amewapongeza wahitimu wote kufanikiwa kumaliza mafunzo hayo ambayo ni muhimu kwa uhifadhi wa maliasili katika maeneo ya vijijini ambako kuna rasimali nyingi za nchi zinazotakiwa kulindwa.
Ujangili hususani wa tembo umekuwa ni changamoto na tishio kwa nchi yetu na ustawi wa rasilimali hizo,licha ya serikali kujitahidi kufanya kila linalowezekana ili kukomesha ujangili huo kwa kweli ujangili wa tembo bado upo,tunataka kufikia sehemu ambayo tunaweza kusema hatuna ujangili Tanzania’’,alisisitiza Milanzi.
Hata hivyo amesema pamoja na mafanikio ambayo serikali imeyapata katika mapambano dhidi ya ujangili,bado ujangili upo sio kwa tembo tu bali hata wanyama wengine wanauawa kwa sumu ambapo Wizara ya Maliasili imepoteza simba katika baadhi ya maeneo kwa kuwa sumu.
Awali akitoa taarifa ya chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili Kwa Jamii (CBCTC) ,Mkuu wa chuo hicho Jane Nyau alisema wanachuo 55 ambao wamehitimu Juni 24,2018,walianza mafunzo Machi 23,2018 wakiwa jumla ya washiriki 56 kati yao wanaume 38 na wanawake 18.
“Washiriki 50 wanafadhiliwa na Shirika la WWF na sita wanafadhiliwa na Shirika la Carbon Tanzania lililoko mkoani Arusha,hata hivyo washiriki 55 ndiyo wametunukiwa vyeti mshiriki mmoja aliahirisha kozi kutokana na matatizo ya kiafya’’,alisisitiza.
Chuo cha CBCTC kilianzishwa mwaka 1995 na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii,lengo likiwa ni kutekeleza sera ya wanyamapori inayosisitiza ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi wa rasilimali za maliasili.
Kwa mujibu wa Mkuu wa CBCTC,chuo hicho kimefanikiwa kuijengea jamii uwezo kwa njia ya mafunzo ili kuiwezesha kushiriki kikamilifu katika uhifadhi na matumizi endelevu ya maliasili ambapo tangu kuanzishwa kwake hadi sasa jumla ya wananchi 4512 wamepata mafunzo kati yao wanaume 3804 na wanawake 708.
Mwandishi ni Albano Midelo
Mawasiliano albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa