HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imeanza utekelezaji wa kutokomeza mbu baada ya kutoa mafunzo maalum kwa wafanyakazi wa kujitolea 49 watakaofanya kazi ya kupulizia dawa hiyo katika mazalio ya mbu yaliowazi na yaliofunikwa.
Mratibu wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa wa Afya na Mazingira katika Manispaa ya Songea Vitalis Mkomela amesema kwa kuanzia zoezi hilo linafanyika katika mitaa 49 iliyopo kwenye Kata kumi za Manispaa hiyo baada ya mafunzo ya nadharia na vitendo kukamilika.
Mkomela anazitaja Kata zinazoanza kupuliziwa dawa za kutokomeza mbu kuwa ni Subira, Matarawe, Majengo, Lilambo, Mletele, Bombambili, Ruhuwiko, Mjini, Mwengemshindo na Mfaranyaki.
Rais amenunua lita laki moja za dawa za kuua mbu na kusambazwa kote nchini ili kukabiliana na malaria.
Viuadudu vya kutokomeza mbu wa malaria vinatengenezwa katika kiwanda cha kuzalisha Viuadudu kilichopo Mjini Kibaha mkoani Pwani.
Halmashauri 14 nchini ikiwemo ya Manispaa ya Songea zina viwango vikubwa vya maambukizi ya ugonjwa wa malaria. Manispaa ya Songea imepokea lita 1000 za dawa hiyo ambapo kiasi hicho cha dawa kinatosha kupulizia kipindi hiki cha kiangazi katika mitaa 95 ya Manispaa hiyo.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa