WIZARA ya Nishati ilizindua mradi wa umeme vijijini Awamu ya tatu katika mkoa wa Ruvuma mwezi Agosti 2017.
Kupitia mradi huo serikali inatarajia kupeleka umeme katika vijiji vyote vya Mkoa wa Ruvuma na kwamba umeme wa Grid ya Taifa unatarajia kufika mjini Songea kabla mwisho wa mwaka huu.
Waziri wa Nishati Dk.Medard Kalemani anaitaja azima ya serikali kuwa ni kusambaza umeme katika vijiji vyote vya mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine kupitia Wakala wa umeme vijijini(REA) ili umeme huo uweze kuchochea maendeleo hadi vijijini.
Dk.Kalemani anavitaja vijiji 440 kati ya vijiji 552 vilivyopo katika Mkoa wa Ruvuma ambavyo bado havina umeme hivyo kupitia mradi wa REA awamu ya tatu vijiji vyote vitapelekewa umeme.
Anasema REA awamu ya tatu imeanza Agosti 2017 ambapo jumla ya vijiji 270 vinapelekewa umeme na kwamba vijiji 140 vinavyobakia vitaanza kupelekewa umeme kuanzia Aprili 2019 na kwamba hadi kufikia mwaka 2021 vijiji vyote katika mkoa wa Ruvuma vitakuwa vimepelekewa umeme.
“REA itapeleka umeme katika vijiji vyote,vitongoji vyote na Taasisi zote za umma zikiwemo shule,vituo vya afya, zahanati, masoko, magereza,misikiti na makanisa yote kwa bei ya shilingi 27,000 tu ya kuingiza umeme,lazima wapeleke umeme nyumba kwa nyumba’’,anasisitiza Dk.Kelamani.
Hata hivyo anasisitiza wananchi kujenga nyumba bora na imara ambazo zinafaa kuingiziwa umeme ambapo na kwamba suala la kupeleka umeme kwa kila nyumba ni la lazima.
“Licha kuhamasisha ujenzi wa nyumba nzuri,haijalishi unaishi nyumba gani,iwe unaishi nyumba ya tembe tunakutundukia umeme humo humo,hata nyumba ya matope tunakutundukia umeme humo humo,tunachotaka umeme utumike na kila mmoja wetu’’,anasema Dk.Kelamani.
Mkandarasi ambaye anafanyakazi ya kujenga mradi wa umeme wa REA awamu ya tatu katika mkoa wa Ruvuma ni NAMIS COOPERATIVE LTD ambayo itafanyakazi katika kipindi cha miezi 24 kuanzia 2017 hadi 2019.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Septemba 13,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa