Kabila la Wamatengo ni Kabila la Asili, halijaundwa kwa kutokana na makabila mengi yaliyochanganyika kama ilivyokuwa kwa kabila la Wangoni, ndio maana hata lugha yake haijaathiriwa na lugha zingine kwa kiasi kikubwa.
Ni makabila machache tu yaliyotoka katika koo nyingine ukoo wa akina KAPINGa, KOMBA (Hanze), MAPUNDA na LUANDA; ni koo ambazo ziliingia kutoka upangwa. Vile vile koo kama akina NDIMBO na NCHIMBI zilitoka Magharibi ya pwani ya ZIWA NYASA. Koo hizi ambazo zilitoka nje hazikuleta athari katika lugha ya kimatengo, ukizingatia kuwa koo hizo zilikuwa chache kiidadi kuliko wenyeji wa asili ya nchi ya UMATENGO.
MAKITA KAYUNI wa ukoo wa akina NDUNGURU ambaye ni Babu kati ya watawala waliokuwa machifu katika nchi ya Umatengo mwishoni inasadikika kuwa, kwa asili alitoka kabila la WANINDi, aliishi chini ya mlima Matogoro karibu na Songea.
Alipoingia MPUTA MASEKO katika nchi ya Ungoni. MAKITA KAYUNI alishindwa kupigana naye akasalimisha jeshi lake kisha akajiunga naye na akapata fursa ya kujifunza mbinu za kivita.
Kayuni alijipatia uhuru wa kufanya chochote na kwenda kokote alikotaka baada ya Mputa Maseko kufukuzwa katika Wilaya ya Songea, akaamua kuhamia katika nchi ya umatengo huko LITEMBO ambako alipokelewa kwa ukarimu mkubwa mno na KAWANILA HYERA pamoja na LIHUHU KINUNDA.
Kayuni alikuwa na ufundi katika masuala vita pamoja na akili ya maisha, watu wa Litembo (Wamatengo) waliona anafaa kuwa kiongozi; alipokufa Kawamila bwana Makita alichaguliwa kuwa mrithi wake.
Baba wa Kayuni Mzee Kapitingana alifika Litembo na kuweka makazi yake; licha ya kwamba Kayuni hakuishi Litembo maisha yake yote lakini alizaliwa katika ardhi ya Litembo kwa Ndenya Ndunguru. Kayuni alipewa jina la ukoo wa Mama yake kwa kuwa Baba yake Mzee Kapitingana hakulipa Mahari.
Familia ya Makita kipindi cha Mputa Maseko (1864 -1865)
Ukoo wa Babu, Baba, Makita na Familia yake waliishi Litembo, familia ya Makita ilifika Litembo baada ya Mputa Maseko kuikimbia Songea mwaka 1864s.
Inaelezwa mwaka 1866s Kayuni alipata bahati ya kuzaliwa; hivyo kuna uhakika kwamba Makita Kayuni aliuawa akiwa na umri mkubwa kwenye vita ya mwisho kati ya Wangoni na Wamatengo ambayo ilikuwa miaka minne kabla ya kifo cha Nkosi Mharule kilichotokea mwaka 1885.
MAKAZI YA WAMATENGO NA TAKWIMU ZAO KABLA YA WANGONI KUJA SONGEA
Kabla ya Wangoni kuja Songea na kujenga Makazi yao, Wamatengo waliishi katika vijiji ambavyo vilitengana tengana au kutawanyika (Musi musi) kama vile Litembo, Mapera, Ungima (Ngima), Hanga, Kitogota, Kimati, Nkuka, Ungwindi, Baruma, Matiri (karibu na Milima ya Lilengalenga).
Wamatengo walipata shida sana kulinda Miji yao dhidi ya vita ya Wangoni walipoelekea umatengoni ili kufanya makazi yao. Kundi kubwa la watu wailishi katika Bonde la Litembo.
Mwandishi Fullborn amefafanua kwamba, kijiji cha Makita kilikuwa na watu 5,000 kwa mujibu wa Sensa iliyofanywa na Wajerumani mwaka 1904 huku idadi kubwa ya watu ikitoka katika bonde la Litembo katika eneo la Makita, suala ambalo lilipelekea ulinzi kuwa mdogo wakati wa vita.
Wageni waliobahati kutembelea katika kijiji cha Makita wanafafanua kwamba mitetemeko yote inayohusiana na milima ya Litembo ilijengwa vibanda, mapango katika milima ya Litembo yalitumika kwa ajili ya kujificha wakati wa vita. Bro. Laurentius Brenner aliyapima baadhi ya mapango mwaka 1906 na akaandika mambo muhimu aliyoyabaini.
ITAENDELEA
©Peramiho Publications
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa