Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli tayari ametangaza kuwa tupo katika vita ngumu ya kiuchumi katika sekta ya madini, ni vita kubwa na hatari zaidi duniani kwa kuwa inayahusu mataifa makubwa yenye uwezo kiuchumi.
Hii ni vita kubwa kwa kuwa Kampuni za uwekezaji katika sekta ya madini zinatoka mataifa ya magharibi yanatumia mbinu mbalimbali kuhakikisha kuwa nchi za Afrika ambazo zina utajiri wa madini zinaendelea kupoteza huku mataifa hayo yakiendelea kuneema na rasilimali za Afrika.
Katika kutekeleza agizo la Rais la kukabiliana na vita ya kiuchumi katika sekta ya madini,Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amefanya ziara kwenye mgodi wa dhahabu wa Buzwagi uliopo wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na kuchukua sampuli za mchanga katika makontena kwa lengo la kwenda kuyapima kwa wataalamu wa madini ili kubaini kiasi cha dhahabu kilichomo.
Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa kuna sababu mbalimbali ambazo zinasababisha Tanzania na nchi mbalimbali za Afrika kuendelea kupoteza katika sekta ya madini.
Rais Magufuli aliteua Kamati maalum ya wajumbe wanane kuchunguza aina na viwango vya madini yaliyomo kwenye mchanga wa madini uliomo ndani ya makontena yaliyozuiliwa na Serikali kusafirishwa nje ya nchi.Uteuzi wa kamati hiyo ulifanywa Machi,29,2017. Wajumbe wa Kamati hiyo ni wana taaluma katika fani za jiolojia, kemia, uhandisi kemikali na uhandisi uchenjuaji madini.
Chimbuko la kufanyika kwa uchunguzi huu ni kutokana na ukweli kuwa viwango vya madini yaliyopo kwenye makinikia havijulikani, na hata mikataba ya uchenjuaji makinikia haipo wazi.Hali hii inaleta hisia kuwa nchi inaibiwa na hainufaiki na uchimbaji wa madini.
Katika kutekeleza uchunguzi huu,Kamati iliongozwa na Hadidu za Rejea zilizoridhiwa na Serikali ambazo ni kufanya uchunguzi kwenye Makinikia yaliyopo Bandari ya Dar esSalaam, Bandari Kavu na migodini kwa kupekua na kubaini vitu vilivyomo ndani na kuchukua sampuli za makinikia ili kuzifanyia uchunguzi wa kimaabara.
Hadidu nyingine ni Kufanya uchunguzi wa kimaabara na kubainisha aina, kiasi na viwango vya madini yatakayoonekana katika makinikia kisha kubainisha thamani ya madini hayo,kutumia mitambo ya scanners iliyopo katika Bandari ya Dar esSalaam kwa ajili ya kujiridhisha na aina ya shehena zilizomo kwenye makontena yenye mchanga wa madini.
Kubainisha uwezo wa scanners hizo kuona vitu vyenye ukubwa na maumbile tofauti vilivyomo ndani ya makontena yenye makinikia, kuchunguza utendaji wa Wakala wa Serikali wa Ukaguzi Madini(TMAA) wa kuchukua sampuli za makinikia,uchunguzi wa madini kwenye maabara na utaratibu wa ufungaji wa utepe wa udhibiti (seal) kwenye makontena kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.
Ili kutekeleza uchunguzi huu,Kamati hiyo ya vita ya kiuchumi katika sekta ya madini ilifanya yafuatayo ,kuandaa mpango kazi, kukusanya nyaraka na taarifa mbalimbali kuhusiana na makontena yenye makinikia yaliyozuiliwa na Serikali kusafirishwa nje ya nchi,kutembelea maeneo yote yenye makontena yenye shehena za makinikia ili kuyachunguza na kuchukua sampuli zake.
Maeneo hayo ni Bandari ya Dar es Salaam, Bandari Kavu – ZAM CARGO na migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi,kutathmini uwezo wa scanners wa kuonesha makinikia yaliyomo ndani ya makontena pamoja na vitu vingine ambavyo vinaweza kuwa ndani ya makinikia.
Kamati hiyo ya Rais pia ilifanya uchunguzi wa kimaabara wa sampuli za makinikia na kubaini aina,viwango na kiasi cha madini yaliyomo kwenye makinikia,kukokotoa thamani ya madini yaliyopimwa kwenye makinikia kwa kutumia viwango vilivyopatikana kutokana na uchunguzi wa kimaabara na thamani ya madini hayo kwenye soko la dunia na kuchunguza utendaji wa Wakala wa Serikali (TMAA) wa kukagua na kudhibiti uzalishaji na usafirishaji wa makinikia.
Vita hii ya Rais imezaa matunda ambapo sasa watanzania wameanza kuona neema katika madini yetu,hivyo basi tumuunge mkono Rais katika Vita hii ngumu ya kiuchumi ili hatimaye watanzania waanza kunufaika katika sekta ya madini,gesi na mafuta.
Makala haya yameandikwa na Albano Midelo,baruapepe albano.midelo@gmail.com
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa