ZIARA ya kushitukiza ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dk.Gozibert Mutahyabarwa imefanyika katika Kliniki za Manispaa ya Songea na kubaini kliniki mbili zinaendeshwa kinyume cha sheria za tiba asili na tiba mbadala.Baada ya ukaguzi wa kina toka katika timu mbili za wataalam wa Afya ngazi ya Mkoa wa Ruvuma na wa Manispaa ya Songea umebaini vituo vya Ndulu Herbal Clinic kilichopo Mahenge na Bethlehemu Samaritan Clinic kilichopo Mfaranyaki Songea vinapima wagonjwa kwa kutumia kipimo cha Qantum Resonance Magnetic Analzer ambacho kimepigwa marufuku na serikali.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amesema vituo vyote vya tiba asilia viliandikiwa barua kutoka Manispaa ya Songea kuacha kutumia kipimo hicho ambacho kinawarubuni wananchi kuwa wanaumwa magonjwa mengi hivyo kulipa gharama kubwa kwa ajili ya matibabu ambazo ni kati ya shilingi 150,000 hadi 300,000.Hata hivyo vituo tiba vya asili vimekaidi na kuendelea kutumia kipimo hicho kupima wagonjwa ambapo utafiti uliofanywa na madaktari ulibaini kipimo hicho kinatoa vipimo vya uongo na hakina viwango vya ubora.
Licha ya kutumia kipimo ambacho kimepigwa marufuku,mapungufu mengine ambayo yamebainika katika operesheni hiyo ni vituo hivyo kutumia watalaam ambao hawana sifa za kuwa madaktari na wahudumu wa afya ambapo kituo cha Betherehemu Samaritan Clinic hakijasajiriwa.Kutokana na mapungufu hayo vituo hivyo vimefungwa kuanzia leo Novemba 10,2017 na mashine walizokuwa wanazitumia zimechukuliwa na Idara ya Afya Manispaa ya Songea.
Hata hivyo vituo hivyo vinaweza kufunguliwa iwapo vitafanyia marekebisho maagizo ya serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuzingatia sheria,kanuni na miongozo ili vituo hivyo vitoe huduma rafiki na salama kwa watumiaji.Dk.Mutahyabarwa amesisitiza kuwa kutokana na ukubwa wa tatizo ziara za kushitukiza zitafanyika katika mkoa mzima wa Ruvuma ili kulinda maisha ya wananchi kutokana na matumizi yasiokuwa salama katika tiba asili na tiba mbadala.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa