VIUMBE Zaidi 35,000 wapo katika hatari ya kutoweka duniani kutokana na athari za uchafuzi na uharibifu wa mazingira ambao unaendele kufanyika kila mwaka.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wakati anazungumza katika kilele cha siku ya mazingira duniani kitaifa ambayo yamefanyika jijini Dar es salaam Juni 5.
“Tunapokata miti hovyo tunakimbiza viumbe walioumbwa na mwenyezi Mungu,hivi sasa duniani inakisiwa kwamba kuna aina za viumbe wapatao 35,000 wapo katika hatari ya kupotea au kutoweka duniani kutokana na uharibifu wa makazi yao’’,anasisitiza Makamu wa Rais.
Amewataka Viongozi wa ngazi zote kuongeza nguvu katika utekelezaji wa Sera, Sheria, Mikakati na miongozo katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
“ Ni muhimu, mipango ya maendeleo katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira ili nchi yetu iwe na maendeleo endelevu”alisema Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais amesema kazi ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa hifadhi ya mazingira unahitaji ushirikiano wa wadau wote kwa ngazi zote.
Maadhimisho ya Kimataifa ya siku ya kilele cha mazingira duniani yamefanyika nchini India katika mji wa New Delhi ya kibeba ujumbe wa kuhimiza kupunguza uchafuzi wa mazingira kutokana na matumizi ya bidhaa za plastiki (Beat Plastic Pollution).
Hata hivyo hapa nchini ujumbe wa siku ya mazingira duniani mwaka huu ni “Mkaa Gharama: Tumia Nishati Mbadala”
Katika maadhimisho hayo Makamu wa Rais alizindua ukuta wa bahari uliopo kwenye barabara ya Barack Obama wenye urefu wa mita 920, ukuta huo ambao umejengwa kuzuia bahari kuingia nchi kavu unakadiriwa kuwa na maisha kati ya miaka 70 mpaka 100 kutoka sasa.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa Viwanda na zipo faida nyingi za hifadhi na usimamizi zitakazotokana na Tanzania kuwa na Viwanda.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manipaa ya Songea
Juni 6,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa