KAMPUNI ya serikali ya China inayoitwa China Sichuan International Cooperation (SIETCO) ipo mjini Songea tayari kuanza ujenzi wa stendi mpya ya kisasa katika eneo la Kata ya Tanga Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
SIETCO imesaini mkataba wa miezi 18 na Halmashauri ya Manispaa ya Songea kujenga stendi mpya ya mabasi katika eneo la Tanga kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.
Mwakilishi wa Kampuni ya SIETCO imeiambia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Songea kuwa, wanatarajia kutoa ajira kwa wakazi wa Songea ambapo hivi sasa tayari wametoa ajira kwa wafanyakazi wachache katika hatua za awali za kuanza mradi huo.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Songea ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema wamefanya ziara ya ukaguzi wa eneo la stendi ambapo wamemkuta Mkandarasi akiendelea kufanya maandalizi ya awali ya ujenzi wa stendi hiyo .
Kaimu Mwandisi wa Ujenzi katika Manispaa ya Songea Mhandisi Nicolous Danda amesema Kampuni hiyo imesaini mkataba ambao unaanzia Machi 25 hadi Septemba 30,2019.
Amesema mradi hadi kukamilika unatarajia kugharimu shilingi bilioni 12 ambapo katika awamu ya kwanza, zitatumika shilingi bilioni sita na kwamba stendi mpya ya mabasi inatarajia kuanza kazi baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya utekelezaji ambayo ni kuanzia Oktoba 2019.
“Ili kuendana na kasi ya ukuaji wa mji,Manispaa iliamua kutenga eneo la kujenga kituo kikuu cha mabasi kuwa Kata ya Tanga ikiwa ni umbali wa takribani kilometa 14 toka mjini Songea’’,anasisitiza Mhandisi Danda.
Anazitaja kazi ambazo zitafanyika katika awamu ya kwanza na pili ya mradi huo kuwa ni kujenga barabara za kuingia na kutoka stendi zenye kiwango cha lami nzito,kujenga mirefeji ambayo itapeleka maji mtoni,ujenzi wa eneo la stendi lenye ukubwa wa meta za mraba 32,914,kuweka taa za barabarani katika eneo lote la stendi,eneo la utawala na kujenga majengo yenye hoteli za kisasa.
“Fedha za mradi wa stendi zimetolewa kupitia Benki ya Dunia,jumla ya hekari 15 zimetwaliwa katika eneo hilo ili kupitisha stendi,ambapo shilingi milioni 32 tayari zimelipwa kama fidia kwa wananchi’’,anasema Mhandisi Danda.
Kampuni ya SIETCO imesaini pia mkataba wa miezi 18 wa ukarabati wa barabara za lami nzito katika manispaa ya Songea zenye urefu wa kilometa 10.3,kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni kumi.Mkataba huo unaanzia Machi 25,2018 hadi Septemba 30,2019.
Fedha za miradi hiyo ya barabara na stendi zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo serikali za mitaa(ULGSP), mpango huo unakusudia kuendeleza miundombinu ya Halmashauri za miji na Manispaa 18 za Tanzania Bara ikiwemo Manispaa ya Songea.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Aprili 5,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa