MBUNGE wa Jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma Dkt.Damas Ndumbaro anawatangazia wakulima na wafanyabiashara wa Manispaa ya Songea na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kuwa safari ya mafunzo ya nchini Poland inatarajia kufanyika Oktoba 9 mwaka huu.
Kulingana na Mbunge huyo amefanya mazungumzo na Balozi wa Poland kuhusiana na taratibu na Visa tangu Julai mwaka huu na kwamba maandalizi ya safari hiyo yanaendelea vizuri.
Dkt.Ndumbaro amesisitiza kuwa hiyo ni fursa adimu kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na kwamba wakiwa nchini Poland watajifunza namna nchi hiyo ilivyofanikiwa katika sekta ya kilimo,pia wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma watatangaza fursa za kilimo,biashara,utalii na uwekezaji zilizopo katika Mkoa wa Ruvuma.
Hata hivyo amesema wafanyabiashara na wakulima wanaotarajia kwenda katika ziara hiyo ya mafunzo ya siku tano hawazidi kumi ambao kila mmoja anatakiwa kuchangia nauli kati ya Dola 800 hadi 1000 na gharama ya malazi na chakula ni kati ya Dola 500 hadi 700.
Mfanyabiashara yeyote ambaye anapenda kwenda katika ziara hiyo anatakiwa kufika katika Ofisi ya Mbunge wa Songea na kuandikisha jina lake kuanzia sasa hadi Septemba 23,2018.Wafanyabiashara hao pia wanatakiwa kuandaa Pasipoti zao za kusafiria kwa ajili ya maandalizi ya VISA.
Nchi ya Poland iliyopo katika Bara la Ulaya inatajwa kuwa ndiyo nchi ambayo inayoongoza katika bara hilo katika uzalishaji wa zao la mahindi ambapo hekta moja inazalisha tani 11 za mahindi.
Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa nchini inayoongoza kwa uzalishaji wa zao la mahindi,hata hivyo changamoto kubwa ni ukosefu wa soko na pembejeo za kilimo hali ambayo inaleta changamoto kubwa kwa wakulima na wafanyabiashara wa mkoa huo.
Mbunge wa Songea mjini Dk.Damas Ndumbaro amesema hali hiyo ndiyo iliyomsukuma Julai mwaka huu kuwaleta watalaam wa kilimo katika Manispaa ya Songea toka nchini Poland wakiongozwa na Kaimu balozi wa Poland nchini Tanzania Dk.Evelina Lubieniecka.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Septemba 18,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa