WAJASIRIMALI wadogo ambao ni wanawake,vijana na makundi maalum katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamepewa mkopo wa milioni 95 bila riba.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Manispaa hiyo Naftari Saiyoloi akizungumza katika hafla ya utoaji wa mkopo huo kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea amesema kiasi hicho cha fedha kinatolewa katika vikundi 59 vya wajasirimali hao.
Amesema kati ya vikundi hivyo,vikundi vya wanawake 30 vimekopeshwa zaidi ya shilingi milioni 30,vikundi vya vijana 19,vimekopeshwa zaidi ya shilingi milioni 37 na vikundi maalum 10 vimekopeshwa zaidi ya shilingi milioni 26.
Hata hivyo Saiyoloi amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2018/2019 kwa robo ya kwanza Manispaa hiyo ilikopesha wajasiriamali wadogo kutoka vikundi 59 kiasi cha shilingi milioni 59.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kutoa asilimia kumi ya makusanyo ya mapato ya ndani kwa kuzingatia sheria namba 37A(2) iliyoagiza mgao stahili kwa makundi yote.
“Naipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza maagizo ya serikali katika utoaji wa mikopo hii katika makundi haya’’,alisisitiza.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji amewaasa wajasirimali wadogo kuirejesha mikopo kwa wakati ili wakopeshwe wajasirimali wengine.
“Mkopo huu unalenga kupambana na adui umasikini,matajiri wote mnaowaona wakubwa leo wakiwemo Dkt.Mengi na wengineo,walianza kama wajsirimali wadogo na hivi sasa ni miongoni mwa matajiri wakubwa Tanzania’’,alisema Mshaweji.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Songea mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt.Damas Ndumbaro amesema amefarijika kuona mabadiliko ya sheria ya fedha namba 37 katika serikali za mitaa kuanza kuwanufaisha wajasiriamali wadogo.
Amesema katika marekebisho ya sheria hiyo yaliofanywa na Bunge mwaka huu,yanamwezesha mjasirimali mdogo wakiwemo wanawake,vijana na makundi maalum kukopeshwa mikopo bila riba.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea katika wilaya ya Songea ndiyo Halmashauri pekee kati ya tatu ambayo inatekeleza kwa vitendo sheria ya kutoa mikopo ya asilimia 10 ya makusanyo ya ndani katika kila robo ya mwaka wa fedha.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Desemba 30,2018.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa