Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Ruvuma kuwakamata na mali zao wote waliosababisha upotevu wa shilingi bilioni 1.7 za Benki ya wananchi Mbinga.
Mndeme ametoa maagizo hayo ofisini kwake mjini Songea, wakati anatoa taarifa ya Tume ya Uchunguzi wa kubaini sababu za kufilisika hatimaye kufungwa kwa Benki ya wananchi wa Mbinga Mei 10,2017.
Mkuu wa Mkoa amesema aliunda Tume hiyo ili kutekeleza maagizo ya Rais John Magufuli ambaye aliagiza uchunguzi kufuatia kufilisika kwa Benki hiyo hali ambayo ilisababisha fedha za wananchi kupotea bila kujua zitalipwa na nani.
“Tume ya Uchunguzi ilianza kazi tarehe 15/4/2019 na baada ya kuchunguza sababu za kufiliska kwa Benki ya wananchi Mbinga,imebaini upotevu wa fedha za wananchi jumla ya shilingi 1,734,844,629.95’’,alisema Mndeme.
Amesema kiasi hicho cha upotevu wa fedha kimetokana na matumizi mabaya ya fedha za ruzuku kutoka ofisi ya Waziri Mkuu katika Programu ya MIVARF shilingi bilioni moja,wizi wa wazi kwenye akaunti za wateja shilingi milioni 62,mikopo kwa watumishi kwa ajili ya siku kuu ya Idi Chrismass shilingi 266,808,423 na mikopo ambayo haijarejeshwa baada ya kufungwa Benki ni zaidi ya milioni 400.
Kutokana na uchunguzi huo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameagiza fedha zote zirudishwe,mali za wahusika wote zikamatwe ili fedha za wananchi zirejeshwe na kwamba wananchi wote ambao walishirikiana na wafanyakazi wa Benki kufanya udanganyifu wachukuliwe hatua.
Imeandikwa na Albano Midelo
Novemba 12,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa