MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji amesema serikali imekubali kulipa fidia ya sh.bilioni 3.3 za ardhi kwa wananchi wa Kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea.Eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya hekari 5000 lilichukuliwa na serikali katika mwaka wa fedha wa 2008/2009 kwa ajili ya eneo maalum la ukanda wa uwekezaji viwanda(EPZA).
Akitoa taarifa katika mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Songea Meya Mshaweji ameliambia Baraza hilo kuwa Kamati Maalum ikiongozwa na Mbunge wa Songea mjini,Mstahiki Meya wa Songea na Diwani wa Kata ya Mwengemshindo walikwenda Dodoma na kufanikiwa kukutana na Waziri wa Fedha ambaye aliahidi serikali kulipa fidia hiyo.
Kwa mujibu wa Taarifa hiyo,Waziri wa Fedha ameahidi serikali katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 italipa fidia ya sh.bilioni 1.5 kwa wananchi wa Mwengemshindo ili kupunguza deni hilo ambalo wananchi wanadai kwa muda mrefu.Wananchi 1181 wa Kata ya Mwengemshindo wanadai fidia ya sh.bilioni 3.3 ambapo hadi sasa serikali imelipa shilingi bilioni mbili za fidia kwa wananchi hao.
Wakichangia taarifa hiyo baadhi ya madiwani wameiomba serikali kulipa fidia hiyo haraka kwa kuwa wananchi wamechoka kusubiri ambapo baadhi ya wananchi wamekufa bila kupata haki yao.Diwani wa Kata ya Mwengemshindo Osimundi Kapinga amesema serikali ilichukua ekari zaidi ya 5000 za wananchi miaka kumi liyopita ambapo hadi sasa fedha za fidia ambazo zimelipwa ni sh.bilioni mbili tu kati ya fedha zaidi ya shilingi bilioni tano ambazo zinadaiwa na wananchi.
Amesema serikali imekuwa inaahidi kila mwaka wa fedha kuwalipa wananchi fidia yao ambapo hadi sasa hakuna utekelezaji hali ambayo imesababisha wananchi,wanadai watachukua ardhi yao na kuanza kuifanyia kazi.“Katika Mkutano Mkuu wa kata uliofanyika hivi karibuni tumeadhimia kuchukua ardhi yetu bila masharti yeyote ili tuweze kuzalisha na kujenga nyumba kwa sababu wananchi wamekata tamaa na kuchoshwa na ahadi ambazo zimeshindwa kutekelezwa’’,alisema Kapinga.
Naibu Meya wa Manispaa ya Songea Yobo Mapunda amekiri kuwa madai hayo ni ya muda mrefu ndiyo maana wananchi wamekata tamaa,hata hivyo amesema anaamini serikali ya CCM ni sikivu italipa madai hayo kabla ya mwaka huu wa fedha kumalizika.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa