MKUU wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Sophia Kizigo ametoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma kuendelea kuwalinda tembo na faru ambao ni rasilimali muhimu kwa Taifa.
Akizungumza siku ya maadhimisho ya tembo na faru ambayo mwaka huu yamefanyika kwenye uwanja wa michezo wa Zimanimoto mjini Songea,Kizigo ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema vita dhidi ya ujangili inatakiwa kuwa endelevu ili wanyama hao waendelee kuongezeka.
Kizigo amesema kulingana na takwimu siku za nyuma tembo na faru katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambayo awali ilifahamika kama Pori la Akiba la Selous,walikuwa zaidi ya 90,000 ambapo hivi sasa wapo 15,000.
“Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya tembo katika hifadhi ya Taifa ua Nyerere inaongezeka,kwa namna ya pekee tunawapongeza askari wa wanyamapori kwa kazi nzuri ya kulinda rasilimali za nchi’’,alisisitiza.
Kizigo ametoa rai kwa watanzania kuachana na vitendo haramu vya ujangili badala yake wafanye kazi halali na kuacha vitendo vya kuwinda wanyamapori ambao ni vivutio vya utalii ambavyo vinaingiza mapato na fedha za kigeni hivyo kuchangia uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Wanyamapori Nasoro Wawa amesema Idara yake inakabiliana vilivyo na vitendo vya ujangili ambapo katika kipindi cha mwaka 2018 hawakuwa na tukio lolote la ujangili katika hafadhi ya Taifa ya Nyerere (selous) na kusisitiza kuwa hatua kali za kisheria zinachukuliwa kwa mtu yeyote amb aye atakamatwa akijihusisha na vitendo vya ujangili.
Ametoa ushauri kwa wanakijiji ambao wanaishi katika mazingira ya hifadhi kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kujenga uzio au kutumia njia mbadala za kuweza kuwafukuza tembo zikiwemo kuwafukuza tembo kwa kutumia pilipili na mafuta chafu .
Imeandikwa na Farida Mussa
Kitengo cha TEHAMA Manispaa ya Songea
Oktoba 2,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa