WANAWAKE Songea waunda vikundi 400 vya ujasiriamali
Tarehe ya kuwekwa: March 21st, 2018
Kutokana na uhamasishaji wa wanawake kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali unaofanyika Songea Manispaa mkoani Ruvuma imesaidia wanawake kuongeza uelewa na kufanya shughuli za kiuchumi.
Katika kipindi cha mwaka 2017/2018, jumla ya vikundi 36 vya wanawake wazalishaji mali vimeundwa na kufanya jumla ya vikundi 400 vya wanawake vya Songea Manispaa.
Afisa Maendeleo ya Jamii katika Manispaa hiyo Naftari Saiyoloi amezitaja Shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa na vikundi hivyo kuwa ni usindikaji, kilimo, magenge, ufumaji, ufugaji na hifadhi ya mazingira.
Kwa mujibu wa Saiyoloi Katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2017 jumla ya vikundi 51 vya wanawake vimepatiwa mikopo midogo midogo yenye masharti nafuu yenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 71 ambapo kila kikundi kimepatiwa kiasi cha fedha kati shilingi milioni moja hadi tatu.
Afisa Maendeleo huyo amezitaja fursa mbalimbali za kiuchumi na namna ya kutumia Rasirimali zilizopo katika kujiletea maendeleo, zikiwemo mfuko wa Maendeleo ya Wanawake WDF, SACCOS, BANK, NA SIDO ambapo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuna jumla ya taasisi za kifedha 25.
“vikundi vya wajasiriamali 51 Manispaa ya Songea vimepatiwa mafunzo mbalimbali ya kujengewa uwezo juu ya ujasiriamali kwa elimu waliyopewa ya usimamizi na uendeshaji wa miradi ya uzalishaji mali, utafiti wa masoko na elimu ya jinsia kupitia Idara ya maendeleo ya jamii kwa kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka2018’’,amesema Saiyoloi.
Kwa upande wakeJoyce Mwanja ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii katika Manispaa hiyo anabainisha Ongezeko la uelewa kutokana na elimu kupitia midaharo ya wanawake na mafunzo mbalimbali yanayotolewa juu ya kutumia mahusiano ya kijinsia kwa maendeleo ya wanawake na wanaume.
Mwanja anabainisha zaidi kuwa kumekuwa na ongezeko la wanawake wanaoshirikishwa katika maamuzi,kupewa haki na kujengea uwezo wa kutambua maswala ya kisheria yanayosaidia kuondokana na mfumo dume na mifumo kandamizi.
Hata hivyo amesema wanawake walio wengi hivi sasa wameelewa haki zao na hatua za kuchukua dhidi ya uhalifu wa aina yoyote kupitia mdaharo na kwamba kumetokomezwa tabia ya kufanya tamaduni za unyago kwa watoto wa kike katika umri mdogo na kupungua kwa mimba za utotoni.