JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limewakamata watu watatu katika soko la vyakula la Lizaboni Manispaa ya Songea wakiwa na vipande 23 vya meno ya tembo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma SACP Gemini Mushy amesema watu hao walikamatwa Mei 25 mwaka huu ambapo majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.
Hata hivyo Kamanda Mushy amesema vipande hivyo vya meno ya tembo vina uzito wa kilogram 60 vikiwa na thamani ya Zaidi ya shilingi milioni 175.
Katika tukio jingine Kamanda Mushy amesema mtu mmoja ambaye amefahamika kwa jina la Emanuel Romwad(39) amefariki dunia kutokana na ajali ya gari iliyotokea Mei 25, katika kijiji cha Mtakuja wilayani Namtumbo.
Amelitaja gari ambalo limesababisha ajali hiyo kuwa ni lenye namba za usajiri T377 CLE aina ya Mitushubishi Rosa mali ya Omary Kangaulaya wa Songea ambalo liliacha njia na kugonga kingo za barabara kisha kusababisha ajali hiyo katika mtelemko wa mto Likonde.
Amesema ajali hiyo imesababisha majeruhi wawili ambao amewataja kuwa ni Hamis Sinkala(32) mkazi wa Mtaa wa Ruvuma Manispaa ya Songea na Tabu Ramadhani(30) mkazi wa Ligera wilayani Natumbo.
Hata hivyo Kamanda Mushy amekitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe wa dereva kushindwa kulidhibiti gari kwenye mtelemko na kwamba dereva alikimbia mara baada ya ajali,na Jeshi la polisi linaendelea kumtafuta.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 27,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa