JUMLA ya watoto 25,544 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamepata dawa za minyoo sawa na asilimia 67.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu kwenye kikao cha kamati ya lishe kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea Afisa Lishe wa Manispaa hiyo Anna Nombo amesema dawa hizo zimetolewa kwa watoto hao katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.
Amesema katika kipindi hicho jumla ya watoto 17,068 wenye umri chini ya mwaka mmoja katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamehudhuria kliniki katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.
kati ya hao,watoto 12 ambao ni sawa na asilimia 1.1 walikuwa na uzito chini ya asilimia 60.
Kwa mujibu wa Afisa Lishe huyo watoto 1733 ambao ni sawa na asilimia 5.1 walikuwa na uzito kati ya asilimia 60 hadi 80 na kwamba watoto 31,391 sawa na asilimia 91.8 walikuwa na uzito kati ya asilimia 80 hadi 100.
“Katika kipindi hicho jumla ya akinamama 6469 walihudhuria kliniki,kati yao 1905 walipata madini chuma sawa na asilimia 29.4 na akinamama 1636 walipata dawa za minyoo sawa na asilimia 25.3’’,anasema Nombo.
Hata hivyo amesema katika kipindi hicho jumla ya watoto waliozaliwa hai ni 2966 kati yao watoto 236 walizaliwa na uzito pungufu wa kilo 2.5 sawa na asilimia nane.
Nombo anabainisha Zaidi kuwa katika kipindi hicho watoto 4209 wenye umri wa miezi kati ya sita hadi 11 walitarajiwa kupata nyongeza ya vitamin A,ambapo watoto 6624 ndiyo waliopata nyongeza ya vitamin A sawa na asilimia 157.
Amesema watoto 37,879 wenye umri wa miezi 12 hadi 59walitarajiwa kupata nyongeza ya vitamin A,hata hivyo ni watoto 15,167 sawa na asilimia 40 ya lengo ndiyo walipewa vitamin hiyo.
Kulingana na Afisa Lishe huyo katika kipindi hicho jumla ya watoto wachanga 4518 walizaliwa na kwamba mama zao walipewa unasihi wa umuhimu wa kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo yaani(EBF).
Akizungumzia ukaguzi wa madini joto,Nombo amesema umefanyika katika kata saba kati ya 21 za Manispaa ya Songea ambapo jumla ya kilo 6654 za madini joto sawa na asilimia 99.5 zilizokaguliwa kwenye maduka ya rejareja zilikuwa na madini joto ya kutosha.
Takwimu za Januari hadi Machi mwaka huu zinaonesha kuwa uwiano wa nyumba zenye vyoo bora katika Manispaa ya Songea ni asilimia 83.6,ambapo asilimia 47.7 ya kaya zina sehemu ya kunawia mikono.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 28,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa