Halmashauri ya Manispaa ya Songea imetekeleza zoezi la utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa Surua katika vituo 40 vinatoa huduma za chanjo ambapo jumla wa watoto 32,272 wenye umri wa miezi 9 hadi 59 wamechanjwa.
Lengo hilo limefanikiwa kwa kufikia asilimia 112% ambapo makisio ya awali ya Halmashauri ilikuwa jumla ya walengwa wa uchanjaji 28,794 kuanzia umri wa miezi 9 hadi 59, ikiwa mafanikio hayo yametokana na uhamasishaji wa jamii kupitia Redio, Matangazo, vipeperushi pamoja na wahudumu wa Afya ngazi ya jamii
Hayo yamejiri wakati wa kikao cha tathimini cha kamati za huduma za Afya Wilaya kilichofanyika tarehe 28 Februari 2024 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea, kwa lengo la kufanya tathimini ya utekelezaji wa Chanjo ya Surua Manispaa ya Songea.
Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile, ametoa wito kwa wataalamu kufuata utaratibu wa kufanyika kwa vikao ambavyo vipo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Serikali ambapo hufanyika kwa ajili ya kupata taarifa na ufanisi wa utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Ndile alibainisha kuwa, Wizara ya Afya, OR - TAMISEMI kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendesha kampeni ya Kitaifa ya kutoa Chanjo ya Surua kwa watoto wote walio katika umri wa miezi 9 hadi 59
Aidha, Kampeni hii ilifanyika Nchi nzima kuanzia Tarehe 15-18 Febuari, 2024 katika Vituo vya kutolea huduma za chanjo na maeneo maalumu yaliyoandaliwa ambapo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea zoezi la utoaji wa chanjo limetekelezwa katika mitaa yote 95.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa