MGANGA Mkuu wa Manispaa ya Songea Dk.Mameritha Basike amewaongoza watumishi wa afya wakiwemo madaktari na wauguzi kujitolea katika mradi wa ujenzi wa kituo cha afya kata ya Ruvuma.
Dk.Basike amewapongeza watumishi hao kujitoa na kuwaasa wakazi wa kata ya Ruvuma na manispaa ya Songea kuwa na moyo wa kujitolea ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
Jumla ya shilingi milioni 400 zinatarajiwa kutumika katika mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Kata ya Ruvuma Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Musa Willison ni Mhandisi wa Ujenzi ambaye anasimamia ujenzi wa kituo hicho cha afya ambapo amesema hatua ya ujenzi hadi sasa imefikia asilimia 15 na kwamba wanatarajia kukamilisha hatua za awali za ujenzi huo Januari mwaka 2019 ambapo ametoa rai kwa wakazi wa kata ya Ruvuma kuwa na moyo wa kujitolea ili ujenzi huo uweze kukamilika kwa wakati.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji ameishukuru serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Magufuli kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ambao amesema ukikamilika utasogeza huduma ya afya jirani na wananchi.
Akitoa taarifa ya mapokezi ya fedha shilingi milioni 400,Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea Dk.Mameritha Basike amesema fedha za ujenzi wa mradi huo zitatumia mwongozo uliotolewa na TAMISEMI ikiwemo utaratibu wa kutumia force account ili kupunguza gharama za ujenzi wa mradi.
Kwa mujibu wa mwongozo wa matumizi ya fedha zinazopelekwa Halmashauri kwa ajili ya ukarabati au ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini,fedha hizo zimelenga kukarabati vituo au kujenga katika maeneo ya vipaumbele.
Dk.Basike anavitaja vipaumbele vilivyowekwa katika mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya cha Ruvuma kuwa ni jengo la upasuaji,wodi ya akinamama,wodi ya watoto, maabara, nyumba ya mtumishi inayojitegemea na chumba cha kuhifadhia maiti.
“Mradi wa kituo cha Afya Kata ya Ruvuma mkataba wake unaanza Julai hadi Novemba 2018,ili kufanikisha ujenzi huo,kamati tatu zinahusika kusimamia ambazo ni Kamati ya Ununuzi,Kamati ya Mapokezi na Kamati ya Ujenzi’’,alisema Dk.Basike.
Kwa upande wake Dkt.Zainab Chaula kwa niaba ya Katibu Mkuu TAMISEMI amewaagiza wakurugenzi nchini kuhakikisha kuwa fedha za ukarabati au ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za Afya hazitumiwi kinyume na malengo na matarajio yaliyokusudiwa na kwamba fedha hizo ziingizwe kwenye mipango ya fedha za maendeleo.
Naye Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Seleman Jafo ametoa miezi mitatu kwa waganga wakuu wa mikoa nchini,kuhakikisha wanakamilisha miradi ya ujenzi wa vituo vya afya na vituo vipya kujengwa.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa